Rupia

  • Shilingi na Rupia kutumika zaidi katika biashara kati ya Tanzania na India

    Tanzania na India zimefikia makubaliano ya kuongeza matumizi ya fedha za nchi husika katika biashara, badala ya kutegemea dola ya Marekani kama ilvyokuwa hapo awali. Azimio hilo limefikiwa katika mazungumzo kati ya Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi ambapo itawezesha kupunguza mfumuko wa bei tofauti na awali ambapo Tanzania ingelazimika kutumia fedha nyingi kupata dola ya Marekani ili kuagiza bidhaa. Utekelezaji wa uamuzi huo ulishaanza kufanyiwa kazi ambapo hadi sasa biashara yenye thamani ya TZS bilioni 125 imefanyika kwa fedha za nchi husika, hatua inayodhihirisha utayari wa nchi zote kutekeleza makubaliano haya, na sasa hatua inayofuata ni kuongeza matumizi ya fedha hizo. Katika hatua nyingine, India na Tanzania zimebadili uhusiano wao kutoka wa kawaida kidiplomasia kuwa wa mkakati, ambapo nchi zote mbili zimeainisha maeneo mahususi ya kushirikiana yenye maslahi kwa pande zote mbili. Tanzania inatarajia kuendelea kunufaika na ushirikiano wake wa kimkakati na India ikizingatiwa kuwa ni nchi ya tano kwa kuwa na uchumi mkubwa duniani, ikiwa imepiga hatua katika sekta za afya, TEHAMA, nishatia, miundombinu, ulinzi na usalama ambazo ni kipaumbele kwa Tanzania. Hadi mwaka 2022, kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kilifikia TZS trilioni 7.7, hivyo kuifanya India kuwa mshirika wa tatu kwa ukubwa katika biashara na mwekezaji wa tano kwa ukubwa nchini Tanzania. Read More