Mfumo wa Elimu
-
Agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan la kuboresha mfumo wa elimu ili kumwezesha muhitimu kujiajiri na kuajiriwa baada ya kumaliza masomo yake limefanyiwa kazi ambapo serikali imekamilisha uandaaji na uidhinishaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 na mitaala katika ngazi ya elimu ya awali, msingi, sekondari na mafunzo ya ualimu kwa lengo la kufanya elimu inayotolewa iendane na wakati. Kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Samia, mitaala iliyoboreshwa imezingatia mahitaji ya sasa ikiwa ni pamoja na kuweka msisitizo katika stadi za karne ya 21 ili kumjengea mhitimu stadi za kuwasiliana, kushirikiana, ubunifu na fikra tunduizi. Aidha, kwa upande wa elimu ya kati na elimu ya juu, mapitio ya programu mbalimbali pia yanaendelea kwa lengo la kuifanya iendane na wakati, vipaumbele vya nchi na mahitaji ya soko la ajira ambapo elimu ya juu programu zaidi ya 300 zitahuishwa au kuanzishwa. Uamuzi huo wa kimageuzi wa Mheshimiwa Rais umetokana na uhalisia kwamba mfumo wa elimu wa sasa umejikita zaidi kwenye elimu ya jumla na kukosa fursa za elimu na mafunzo, mitaala kutokidhi mahitaji ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia, mfumo usio fanisi wa udhibiti na ithibati ya elimu na upungufu wa nguvu kazi. Kwa maboresho hayo ambayo yataanza kutekelezwa mwaka 2027, elimu ya lazima itakuwa ya miaka 10 badala ya saba kama ilivyo sasa, ambapo mtihani wa darasa la saba utafutwa na badala yake kuanza kufanyika kwa tathimini darasa la sita kwa ajili ya kujiunga na elimu ya lazima ya sekondari. Serikali itatoa na kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo katika elimu ya msingi na sekondari ili kufanikisha upimaji wa matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji unaofanana, pia itaweka utaratibu wa kubaini na kuendeleza wanafunzi wenye vipaji na vipawa mbalimbali. Read More