Maonesho ya Kimataifa ya Mboga na Matunda

  • Maonesho ya mboga na matunda Qatar kufungua fursa kwa wakulima wa Tanzania

    Doha- Qatar: Oktoba 2 mwaka huu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki uzinduzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Mboga na Matunda (Doha International Horticulture Expo 2023) ambayo yanatoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kujifunza na kuwekeza katika kilimo, hususani kwenye teknolojia rafiki ya mazingira. Kazi kubwa ya kuimarisha sekta ya mboga na matunda inayagusa moja kwa moja maisha ya vijana na wanawake ambao ndio wanufaika wakubwa wa ajira takribani milioni 6.5 zinazotokana na sekta, hivyo kuwa na mchango mkubwa katika ukuzaji wa uchumi wa familia na taifa kwa ujumla. Ushiriki wake kwenye jukwaa hilo la kimataifa ni mwendelezo wa mageuzi ya kilimo aliyoyaanzisha nchini ambapo Serikali ya Tanzania kupitia taasisi zake mbalimbali na sekta binafsi inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutafuta masoko ya mazao ya kilimo pamoja na kuvutia uwekezaji kwenye sekta hiyo iliyoajiri zaidi ya asilimi 65 ya Watanzania. Mkakati wa Mheshimiwa Rais ni kuona kilimo kinakuwa kwa wastani wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, ambapo mbali na kufungua fursa za masoko kimataifa, hatua nyingine za kimkakati alizochukua kutimiza lengo ni pamoja na upatikanaji wa mbegu bora, miundombinu ya umwagiliaji, utafiti na upatikanaji wa mbolea nafuu na viuatilifu. Juhudi hizi zinalenga kupunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima na kuongeza tija na uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula nchini na kuiwezesha Tanzania kuuza chakula nje, ikiendelea ushiriki wake katika kuongeza usalama wa chakula duniani na kutunza mazingira kwa wakati mmoja. Read More