Kahawa ya Tanzania
-
Wafanyabiashara wa kahawa kutoka Tanzania wanaolengeka kuuza kahawa katika soko la China wametakiwa kujisajili kupitia Wizara ya Kilimo nchini Tanzania, ili kukidhi vigezo vya kulifikia soko hilo. Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amenukuliwa akisema kuwa mabadiliko hayo yatarahisisha usajili wa kampuni za Tanzania zenye nia ya kuuza kahawa katika soko la China ambapo awali kampuni nyingi zilikuwa zikipata changamoto kufanya usajili katika mtandao wa Mamlaka ya Forodha ya China (GACC). Hatua hii ni mwendelezo wa fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo Tanzania inaendelea kuzipata tangu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara nchini China ambapo akiwa na mwenyeji wake, Rais Xi Jinping walishuhudia utiaji saini mikataba 15 ya kimkakati inayolenga kuimarisha ushirikiano, biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili. Hadi sasa kampuni saba zimeshasajiliwa kuingiza kahawa nchini China ikiwa ni pamoja Kilimanjaro Cables (T) Limited, Cotacof Limited, Taylor Winch Tanzania Limited, Dorman (Tanzania) Ltd, Kamal Agro Limited, Redloong Investment Company Limited na Ibero Coffee Trading Company (T) Limited. Uhakika wa soko la kahawa unaweka uhakika ajira na kuzalisha ajira zaidi kupitia mnyororo wa uongezaji thamani kahawa, soko la uhakika kwa wakulima na kuongeza mapato ya Serikali kwa kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi. Wakati Tanzania ikilenga kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 65,235 mwaka 2021/2022 hadi tani 72,000 mwaka 2022/2023, wakati huo huo inalenga kuongeza mauzo yake ya kahawa nchini China na mipango inaendelea kwa wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki katika Maonesho ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika yanayotarajiwa kufanyika Juni 2023 huko Hunan. Read More