Elimu ya Juu
-
Wanafunzi 640 wanatarajiwa kunufaika na mpango wa ufadhili wa masomo ya chuo kikuu, Samia Scholarship, utakaoanza mwaka wa masomo 2022/23 kwa kutoa ufadhili wa asilimia 100 kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi na hisabati kwenye mtihani wa kidato cha sita. Licha ya kuwa wanafunzi 640 (wavulana 396 na wasichana 244) wamekidhi kigezo cha ufaulu cha kupata ufadhili, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeainisha vigezo vingine vitakavyozingatiwa ambavyo ni; 1. Lazima awe Mtanzania 2. Awe amefaulu ufaulu wa juu katika mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2022 iliyoendeshwa na NECTA katika tahasusi za sayansi (PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN). 3. Mwombaji awe amepata udahili kusoma fani ya teknolojia, hisabati, uhandisi na elimutiba katika chuo kikuu kinachotambuliwa na Serikali hapa nchini. 4. Aombe ufadhili kwa usahihi kwa njia iliyoelekezwa. Mpango huu utakuwa na manufaa mbalimbali ambayo ni; 1. Kuchochea ari ya wanafunzi kupenda na kusoma masomo ya sayansi 2. Kutoa ahueni kubwa wazazi ambao pengine wangelazimika kuuza mali zao ili kumudu gharama za kusomesha watoto fani za sayansi. 3. Kukuza sekta ya sayansi na teknolojia nchini ili kunufaika zaidi na mapinduzi ya nne ya viwanda. 4. Kuongeza idadi ya wasichana/wanawake kwenye fani za sayansi ambao wamebaki nyuma kutokana na mifumo na imani potofu za jamii. Ufadhili huo ambao utazingatia vigezo vya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) utagharamia maeneo yafuatayo; Ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, posho ya vitabu na viandikwa, mahitaji maalum ya vitivo, mafunzo kwa vitendo, tafiti, vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na bima ya afya. Wanafunzi watakaofadhiliwa watagharamiwa kwa miaka mitatu hadi mitano kulingana kila mmoja programu aliyodahiliwa, na atatakiwa kuwa na ufaulu usiopungua GPA ya 3.8 katika mwaka wa masomo ili kukidhi kigezo cha kuendelea na ufadhili. Read More