BoT
-
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu anaendeleza mageuzi chini ya falsafa ya 4R ambapo katika muktadha huo leo Benki Kuu Tanzania (BoT) imetangaza riba elekezi ya asilimia 5.5 ya benki kuu (CBR) kwa benki zote zinazokopa katika benki hiyo ambayo itakatumika kwa robo ya kwanza ya mwaka 2024 kuanzia leo. Mabadiliko hayo yamefuatia taarifa ya BoT ya Januari 3 mwaka huu ambapo ilitangaza kuanza kutumia mfumo unaotumia riba katika kutekeleza Sera ya Fedha, badala ya mfumo unaotumia ujazi wa fedha, mabadiliko ambayo yanalenga kuongeza ufanisi wa sera ya fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha shughuli za kiuchumi. Utofauti wa mfumo wa zamani na wa sasa wa utekelezaji sera ya fedha (hyperlink) Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema kiwango hicho cha riba kimezingatia lengo la kuhakikisha thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni inaendelea kuwa imara na kinaendana na malengo ya kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 5 na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia lengo la asilimia 5.5 au zaidi kwa mwaka 2024. Kupitia mfumo mpya, pamoja na mambo mengine BoT inatekeleza majukumu yake kwa kupandisha au kushusha kiwango cha riba kwa mikopo kwenda benki za kibiashara, ili kuongeza au kupunguza fedha kwenye mzunguko, kudhibiti mfumuko wa bei, kuimarisha thamani ya shilingi au kukabiliana na changamoto nyingine ya kiuchumi kwa wakati husika. Mfumo unaotumia riba unatumika katika nchi zote za Afrika Mashariki kama sehemu ya mkakati wa kuwa na sarafu moja na benki kuu moja ya Afrika Mashariki, pia unatumika katika jumuiya nyingine za kiuchumi ambazo Tanzania ni mwanachama. Read More