Biashara Tanzania na India
-
Azma ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji inazaa matunda ambapo Tanzania na India zimefikia makubaliano ya kibiashara ambayo yatawezesha wafanyabiashara kutoka pande zote kutumia fedha zao (shilingi na rupia) katika kufanya miamala ya kibiashara. Nafasi hii itarahisisha biashara ambapo India ni moja ya washirika wakubwa wa kibiashara na Tanzania ambapo thamani ya biashara kati ya nchi hizi ni TZS trilioni 10.4 katika mwaka ulioishia Machi 2022. Takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka wa kwanza wa Rais Samia, India iliingiza nchini bidhaa zenye thamani ya TZS trilioni 5.3, huku ikipokea bidhaa za TZS trilioni 5.1 kutoka Tanzania. Utaratibu huu mpya si tu utakuza biashara kati ya mataifa haya kufikia lengo la zaidi ya TZS trilioni 13.8 mwaka huu, bali pia utaziwezesha kutunza akiba ya fedha za kigeni ambao sasa hazitahitajika kufanya miamala. Watanzania wanaofanya kazi katika sekta za kilimo na madini watanufaika zaidi kutokana na sekta hizo kuingiza bidhaa zaidi nchini India. Kwa mujibu wa wachumi na wataalamu wa biashara, uamuzi huo pia utaimarisha utabirikaji wa viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni jambo ambalo ni la muhimu sana katika biashara za kimataifa kwani ina usimamizi wa fedha yake tofauti na awali ilipokuwa ikitumia dola za Marekani. Read More