Mama Yukokazini

  • Mageuzi ya Rais Samia yaongeza gawio la mashirika ya umma hadi bilioni 900

    Moja ya ‘R’ katika falasafa ya 4R ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawakilisha’Reforms’ (Mabadiliko) ambapo amelenga kutoa fursa zaidi kwa watu wengi zaidi kunufaika kiuchumi badala ya wachache. Matokeo ya mabadiliko hayo kiuchumi tunaendelea kuyashuhudia ambapo mabadiliko yaliyofanywa kwenye uendeshaji wa mashirika ya umma umeongeza gawio linalotolewa kwa Serikali kwa mwaka 2024/25. Gawio hilo limeongeza kwa asilimia 40 toka TZS bilioni 633.3 mwaka 2023/24 hadi zaidi ya TZS bilioni 900 iliyokusanywa hadi sasa ambapo lengo ni kukusanya TZS trilioni 1 kabla ya Juni 10 mwaka huu ambapo gawio hilo litakabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais. Aidha, mabadiliko hayo si tu yameongeza gawio bali pia yameongeza mashirika yanayotoa gawio ambapo kwa mwaka huu ni zaidi ya 200 ikilinganishwa na wastani wa mashirika 146 kuanzia mwaka 2021/22 hadi mwaka 2023/24. Mageuzi yaliyofanywa ikiwemo kuyapa uhuru na kuyawezesha kujiendesha kibiashara yamewezesha mashirika yaliyokuwa yanapata hasara kuanza kupata faida. Mageuzi mengine ni kuunganishwa kwa taasisi 14 na kufutwa kwa taasisi nyingine, kuongeza uwazi na uwajibikaji pamoja na ufanisi katika kutathmini bodi za wakurugenzi. Haya ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita kwani yanaipunguzia serikali mzigo wa kuhudumia taasisi hizo kwa kuzipa ruzuku, lakini pia kunaleta tija ya kuanzishwa kwa taasisi hizo hasa katika kuwahudumia wananchi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Read More

  • Ilani ya CCM (2025-2030) imebeba ajenda zinazogusa maisha ya wananchi

    Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ndugu Samia Suluhu Hassan Mei 30 mwaka huu ameongoza chama hicho kuzindua Ilani ya Uchaguzi (2025-2030) ambayo imebeba ajenda tisa, ambazo ni matamanio ya wananchi ambayo wamekuwa wakitaka kuona serikali ikiyafanyia kazi ili kuboresha maisha yao na kuchochea maendeleo ya Taifa. Katika kipindi hicho cha miaka mitano, lengo kuu la serikali litakuwa kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi. Ili kufikia lengo hilo, mkazo mkubwa utawekwa katika maeneo tisa ambayo ni, kuchochea mapinduzi ya kiuchumi, kuzalisha ajira, kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kukuza matumizi ya sayansi na teknolojia, kudumisha amani, utulivu na usalama, kudumisha utamaduni na kukuza sanaa na michezo na kuongeza kasi ya maendeleo vijijini. Ni wazi kuwa, maeneo yote tisa yanagusa maisha ya wananchi, na hili linadhihirisha dhamira ya Dkt. Samia katika kuendelea na mageuzi kwa lengo la kutokomeza umaskini, kuinua hali za maisha ya Watanzania wote na kuinua ustawi wa jamii na Taifa letu. Amewahakikisha wananchi kuwa, kutokana na mafanikio makubwa ambayo CCM imeyapata katika utekelezaji wa ilani ya mwaka 2020-2025, ni wazi kuwa inauwezo wa kutekeleza ilani mpya, ambayo imetengezwa kwa weledi mkubwa ikijumuisha maoni ya wananchi na wadau mbalimbali pamoja na mapendekezo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. “Kubwa kwa Watanzania, ni kuweka utulivu ndani ya nchi yetu, kufanya kazi kwa bidhii,” amesema Dkt. Samia huku akiwaasa wananchi kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kufanikisha yote waliyojipangia. Wananchi na taasisi zilizotoa maoni yao kuhusu ilani hiyo wamekipongeza chama hicho kuwa kimezingatia maoni yaliyotolewa, ambayo kwa muda mrefu yalikuwa ni matamanio ya wananchi ikiwemo suala la Katiba Mpya ambapo chama hicho kimeahidi kuhuisha na kukamilisha mchakato wa katiba hiyo. Read More

  • MAMA aboresha Sera ya Mambo ya Nje ili kukuza Diplomasia ya Uchumi na kulinda utamaduni wetu

    AKIAHIDI, ANATIMIZA. Hayo ndiyo maneno mawili yanayoweza kutumika kueleza tukio la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzindua Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 (Toleo la Mwaka 2024), ambayo ni ahadi aliyoitoa Aprili 2021 wakati akihutubia bunge, mwenzi mmoja baada ya kuingia madarakani. Akizungumza bungeni alisema kuwa serikali itaifanyia maboresho sera hiyo ili iendane na mabadiliko ambayo yametokea ndani na nje ya nchi katika sekta mbalimbali. Ikiwa ni miaka 24 tangu kupitishwa kwa sera hiyo, leo Mei 19, 2025 Mheshimiwa Rais amezindua toleo hilo ambalo limejikita katika Diplomasia ya Uchumi likilenga kulisukuma Taifa mbele na kuimarisha ushiriki na ushindani katika siasa na maendeleo ya kimataifa, kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania kupitia diplomasia makini na shirikishi. Toleo la mwaka 2024 limeleta maboresho mbalimbali ambayo ni pamoja na kuongeza msingi mmoja (wa nane) katika Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Msingi huo ni kulinda na kuendeleza maadili, mila na utamaduni wa Mtanzania ikiwemo kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili, hatua ambayo inalenga kukabiliana na uvamizi mkubwa wa utamaduni na ustaarabu unaoendelea. Aidha, mambo mengine manne yaliyoongezwa ni, moja, kuimarisha Diplomasia ya Uchumi kwa kuvutia uwekezaji wa mitaji mikubwa, kutumia vizuri fursa ya kijografia tuliyojaliwa na kufaidika na soko huru la biashara Afrika. Pili, ni matumizi ya lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya kujenga ushawishi ili kupanua masoko ndani na nje ya Afrika. Tatu, kukuza ushiriki wa Diaspora katika kukuza uchumi wao binafsi na uchumi wa taifa, na nne ni kuangalia fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi ikiwemo uchumi wa buluu ili kuchochea ukuaji wa kiuchumi. Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wote walioshiriki kuandaa sera hiyo, hasa wananchi waliotoa maoni akisema kuwa “mmeshiriki katika kujenga hatma ya nchi yenu na mmeweka alama isiyofutika.” Read More

  • DP World yaongeza mapato Bandari ya Dar kwa zaidi ya TZS trilioni 1

    Falsafa ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reform, and Rebuild) ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuleta mageuzi katika sekta mbalimbali zinazogusa maisha ya Watanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchini. Moja ya sekta hizo ni uchukuzi, ambapo Mageuzi (Reform) yaliyofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuingia ubia na Kampuni za DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL) katika kuendeleza na kuendesha baadhi ya maeneo ya bandari hiyo yameendelea kuleta matokeo, ikiwemo kuongeza mapato. Kati ya Julai, 2024 hadi Februari 2025, mapato yatokanayo na Kodi ya Forodha kutoka bandarini yanayokusanywa kutokana na shughuli za kibandari yamefikia TZS trilioni 8.26, ambalo ni ongezeko la TZS trillion 1.18 ikilinganishwa na makusanyo ya TZS trilioni 7.08 yaliyokusanywa kipindi kama hicho kwa mwaka 2023/24. Mafanikio hayo yametokana na wawekezaji hao kuwezesha upatikanaji wa vifaa na mitambo ya kisasa na mifumo ya TEHAMA inayoendelea kuleta ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za kibandari, hasa kuondoa msongamano wa mizigo na foleni za meli, hali inayochochea wafanyabiashara zaidi kuchagua kutumia bandari hiyo, hivyo kuongeza mapato. Lengo la Mheshimiwa Rais Samia kushirikisha sekta binafsi ni kuongeza tija katika utendaji wa bandari nchini ili kuziwezesha zichangie zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu na maendeleo ya wananchi kwa ujumla kwa kuwafanya wanufaike na rasilimali za nchi yao. Read More

  • MAMA akamilisha miradi ya maji zaidi ya 2,000; mamilioni ya wananchi wapata maji safi

    Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali nchini ambapo katika sekta ya maji, ndani ya kipindi cha miaka minne amekamilisha miradi ya maji zaidi ya 2,331 mijini na vijijini ambayo imefikisha maji kwa mamilioni ya wananchi. Kutokana na ufanisi huo asilimia 83 ya wakazi wote wa vijijini wanapata maji safi na salama ikiwa ni ongezeko toka asilimia 72.3 alizokuta wakati anaingia madarakani Machi 2021. Aidha, kwa sasa asilimia 91.6 ya wananchi wa mijini wanapata huduma ya maji safi na salama ikilinganishwa na wastani wa asilimia 86 aliyoikuta. Mafanikio haya yanakaribia lengo lililoanishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025) ambayo inaielekeza serikali kuongeza kasi ya usambazaji majisafi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya asilimia 85 vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini, kwa upande wa Tanzania Bara, ifikapo Desemba 2025. Ili kuhakikisha lengo la ilani, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji 1,544. Hatua hii inadhihirisha dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais kufikisha maji kwa kila mwananchi popote alipo akitambua kuwa maji ni uhai, maendeleo na usalama kwa wananchi. Read More

  • Mama ashusha neema kwa watumishi wa umma; kima cha chini cha mshahara ni laki 5

    Ni furaha furi furi kama sio furaha bojo bojo kwa watumishi wa umma na Watanzania kwa ujumla baada ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 35.1. Kutokana na nyongeza hiyo, kima cha chini kuanzia Julai 1, 2025 kitakuwa TZS 500,000 toka kiwango cha TZS 370,000 cha sasa. Mheshimiwa Rais ametangaza neema hiyo katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Dunia (Mei Mosi) ambayo kitaifa imefanyika mkoani Singida ikiwa na kaulimbiu isemayo, “Uchaguzi Mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi wote, sote tushiriki.” Amesema nyongeza hiyo ni sehemu ya hatua ambazo serikali yake imeendelea kuchukua kuleta ustawi kwa wafanyakazi nchini, na kwamba uamuzi huo umewezeshwa na kasi ya ukuaji wa uchumi kupanda hadi kufikia 5.5% kwa mwaka, hali iliyochangiwa na wafanyakazi kujituma na kufanya kazi kwa bidii. Kupitia mitandao ya kijamii wananchi wamefurahia nyongeza hiyo ambapo wameandika jumbe za kumpongeza. Baadhi ya jumbe hizo ni; “Nakuamini na nakupenda sana mama maisha yangu yote sijawahi kupiga kura ila mwaka huu inshallah nna Imani kura yangu unayo ya kwanza kwenye maisha yangu,”- Hamoud Jimia. “Ubarkiwe mama ikulu yako huna mpinzani hata kidgo,”- Kisila Legandy “Safi mama Samia, wewe ndo unatudai na tunakuhakikishia lazima tukulipe,”- Julius Peter “Kima cha chini cha mashahara kinapanda kutoka 300k mpaka 500k nomaa,”- Msaki. Kuhusu sekta binafsi Mheshimiwa Rais amesema kuwa Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara inaendelea na tathmini kwa lengo la kuboresha viwango vya mishahara kwa sekta binafsi. “Tutaendelea kuboresha mazingira ya wafanyakazi ikiwemo maslahi ya wafanyakazi kwa kadiri hali itakavyoruhusu… Ili tuweze kujenga vyema Taifa letu ni lazima tulinde amani na utulivu nchini,” amesisitiza Rais Dkt. Samia. Read More

  • Isome hapa hotuba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu katika Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania

    Isome hapa hotuba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania. Read More

  • Tanzania imevunja rekodi ya makusanyo ya juu zaidi ya kodi tangu kuanzishwa kwa TRA

    Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA imevunja rekodi ya makusanyo tangu kuanzishwa kwake kwa kukusanya Shilingi Trilioni 3.587 kwa Mwezi wa Desemba sawa na asilimia 103.52 ya lengo ambalo lilikuwa ni kukusanya Shilingi Trilion 3.465. Makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 17.59 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi Trilioni 3.050 zilizokusanywa mwezi Desemba mwaka 2023. Taarifa iliyotolewa TRA imeeleza kuwa mbali na kuvuka malengo ya Mwezi Desemba katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 (Oktoba-Desemba 2024) imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 8.741 sawa na ufanisi wa asilimia 104.63 ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 8.354 ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 19.05 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi Trilioni 7.342 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2023/24. Vilevile TRA imeandika rekodi mpya ya kuweza kufikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi sita mfululizo katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025. Kamishna Mkuu wa TRA Bwn. Yusuph Mwenda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa miongozo mizuri iliyowawezesha kukusanya kodi kwa hiari na kuvuka malengo. Read More

  • Wanafunzi wote 974,332 kujiunga na kidato cha kwanza 2025.

    Serikali imetangaza wanafunzi wote 974,332 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2025 bila kusubiri machaguo kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita. Kwa miaka kadhaa iliyopita ilizoeleka wanafunzi waliohitimu darasa la saba aidha kushindwa kujiunga au kujiunga na elimu ya sekondari kwa mafungu kutokana na sababu mbalimbali lakini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan suala hilo limefikia ukomo. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI wanafunzi wote waliofaulu wataanza masomo kwa wakati mmoja ikiwa ni matokeo ya maandalizi ya mapema yaliyofanywa na Serikali ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2024 wanajiunga na elimu ya sekondari ifikapo Januari 13, 2025. Miongoni mwa shughuli za maandalizi zilizofanyika ni kujenga na kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa, nyumba za walimu pamoja na uwepo wa madawati na walimu wa kutosha ikikukmbukwa kuwa serikali imetangaza ajira mpya za walimu 3,633 hivi karibuni. Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wasichana ni 525,225 na wavulana ni 449,107. Read More

  • Rais Samia akutana na viongozi wa Ngorongoro, kuunda Tume mbili

    Jumapili, Desemba mosi, 2024 katika Ikulu ndogo ya Arusha, Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa na wa kimila wa jamii ya Kimaasai (Malaigwanani) wanaoishi eneo la Ngorongoro na maeneo ya jirani. Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwepo kwa malalamiko dhidi ya baadhi ya maamuzi ya Serikali yanayohusu eneo la Ngorongoro. Katika mazungumzo hayo Rais Dkt. Samia amesema ataunda Tume mbili ambapo moja itachunguza na kutoa mapendakezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro na nyingine itaangalia utekelezaji wa zoezi zima la uhamiaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Rais Dkt. Samia amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na jamii hiyo huku pia akisisitiza ulazima wa wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji miradi inayopita kwenye maeneo yao. Aidha, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye Serikali inayowahudumia Watanzania wote. Hivyo, ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la  Ngorongoro.   Read More