Sekta ya uwekezaji nchini Tanzania imeendelea kuimarika ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2025/26 (Julai – Septemba) kumeshuhudiwa ongezeko la miradi ya uwekezaji, thamani yake na ajira zitakazotokana na uwekezaji huo.
Katika kipindi hicho, Tanzania imesajili miradi 201 ya uwekezaji, yenye thamani ya shilingi trilioni 6.2 ambapo inatarajiwa kuzalisha ajira 20,808. Ufanisi huu unathibitisha kuimarika kwa imani ya wawekezaji nchini, ikiwa ni matokeo ya uongozi bora na mabadiliko ya kisera na kikodi yaliyotekelezwa na serikali.
Sekta ya uzalishaji wa viwandani imeongoza kwa kuvutia miradi mingi (85) ikifuatiwa na majengo ya biashara (30), usafirishaji (29), utalii (24) na kilimo (13). Uwekezaji viwandani umeendelea kuongoza kwa idadi kubwa ya miradi na uzalishaji wa ajira, sambamba na azma ya serikali ya kuchochea mapinduzi ya uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa kuongeza thamani rasilimali zinazozalishwa nchini.
Katika hatua nyingine, miradi inayomilikiwa na wazawa imeongezeka kufikia 74 kutoka miradi 70 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2024/25. Hatua hii inaonesha kuwa mageuzi yaliyofanyika si tu yanawanufaisha wageni, bali pia wazawa ambao ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi.
Umoja wa Falme za Kiarabu ndiyo nchi iliyoongoza kwa uwekezaji nchini kwa kipindi hicho ikiwa na miradi ya TZS trilioni 1.2 ikizitangulia China (TZS trilioni 1.1), India (TZS bilioni 432.5), Singapore (TZS bilioni 342.5) na Ufaransa (TZS bilioni 250.4). Uwekezaji huu unaifanya Tanzania kuendelea kuwa lango la biashara, uwekezaji na usafirishaji katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.