Dira 2050 ni Dira ya Wananchi: Mheshimiwa Rais awahakikisha kuwa itatekelezwa kwa umakini

Kwa mara ya pili katika historia ya Tanzania, tumeandika na kuzindua Dira ya Taifa ya Maendeleo ya miaka 25 (2025-2050) ambayo haifungamani na chama cha kisiasa ambapo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kuwa Rais wa pili kufanya hivyo, baada ya Hayati Benjamin Mkapa aliyeandika Dira 2025 (2000-2025).

Dira hiyo ambayo ni maoni ya wananchi, hasa vijana, inaanzisha safari ya mabadiliko makubwa, ili ifikapo katikati ya karne ya 21 (mwaka 2050) Tanzania iwe nchi yenye ustawi, usawa na uwezo wa kujitegemea. Msingi wa dira hiyo ni maendeleo ya watu yanayochochewa na uchumi imara, wenye ushindani na kipato cha juu, ili kuinua viwango vya maisha ya wananchi na kuondoa umasikini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa dira jijini Dodoma, Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa baada ya kuandikwa na kuzinduliwa, hatua inayofuata sasa ni utekelezaji na kwamba ipo haja ya kufanya mabadiliko ya kifikra, kimtazamo na kimatendo ili kufanikisha malengo yaliyowekwa. Pia, amewasihi wananchi kufanya kazi kwa bidii, ari na nguvu, huku akibainisha kuwa sekta binafsi itapewa nafasi kubwa katika kufanikisha malengo na shahaba tuliyojiwekea.

“Kutokana na uzoefu tulioupata katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya muda mrefu, tumedhamiria sasa kuitekeleza Dira 2050 kwa umakini mkubwa,” ameeleza Mheshimiwa Rais huku akiwahakikisha wananchi kuwa utekelezaji wa dira hiyo utafanikiwa.

Dira hiyo imechagua sekta tisa za mkazo ambazo ni kilimo, viwanda, ujenzi, madini, utalii, uchumi wa buluu, huduma za kijamii, huduma za kifedha na michezo na ubunifu. Sekta hizo zimepewa kipaumbele kutokana na uwezo wake wa kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine.

Baadhi ya malengo mahsusi ya dira ni kuwa nchi yenye kipato cha kati ngazi ya juu, ikiwa na pato la taifa la dola za Marekani trilioni moja, na wastani wa pato la mtu mmoja la dola za Marekani 7,000 kwa mwaka.