Sekta ya Utalii nchini imeipita dhahabu kwa kuwa ya kwanza katika kuingiza fedha za kigeni nchini, ambapo mapato yake kwa mwaka ulioishia Mei 2025 yamefikia dola za Marekani bilioni 3.92 (TZS trilioni 10.2), ikiwa ni asilimia 55 ya mapato yote ya mauzo ya nje.
Kiwango hicho ni ongezeko kutoka dola za Marekani bilioni 3.63 kwa kipindi kama hicho mwaka jana. Ongezeko hilo limeipita dhahabu ambayo imeingiza dola za Marekani bilioni 3.83 (TZS trilioni 9.9), na hivyo kuthibitisha ukuaji madhubuti wa sekta ya utalii na mchango wake katika uchumi wa nchi.
Mafanikio haya ni matokeo ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akitambua umuhimu wa sekta hii katika uchumi wetu ambayo inachangia asilimia 17.2 katika Pato ghafi la Taifa, inachangia asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni na kuajiri zaidi ya milioni 3.
Moja ya hatua iliyochukuliwa ni Julai 8 mwaka huu ambapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliruhusu kampuni za utalii kutumia fedha za kigeni katika maeneo mawili muhimu: wakati wa kulipia bidhaa na huduma kwa niaba ya watalii wasiokuwa wakazi, na wakati wa kununua magari maalum ya utalii kutoka kwa wasambazaji wa ndani.
Uamuzi huo ulipokelewa kwa furaha na Chama cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO) kikieleza kuwa serikali imedhamiria kukuza sekta hiyo yenye mnyororo mrefu wa thamani na kwamba wataendelea kushirikiana nayo ili kuikuza zaidi sekta hiyo.