Kazi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwatumikia Watanzania na kuchochea mageuzi kwenye kila sekta inaendelea kutambuliwa ndani na nje ya nchi ambapo leo amepokea Tuzo ya Wanawake 100 wenye Nguvu Afrika (The Power of 100 Africa Women Award) kutoka Access Bank Group.
Tuzo hiyo ina malengo makuu matatu ambayo ni kutambua na kusherehekea wanawake wa Kiafrika wanaotoa michango ya mageuzi kwa mataifa na jamii zao, kuhamasisha na kuhimiza kizazi kijacho cha viongozi Wanawake katika bara zima la Afrika na kupaza sauti za Wanawake katika kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.
“Mheshimiwa Raisi, leo hii, tunaungana na Waafrika wote kukukabidhi tuzo hii maalumu […] kama kiongozi wa kuigwa ambaye utawala wake shirikishi, mageuzi ya kiuchumi, na utetezi wa jinsia unaendelea kuinua mamilioni ya watu, siyo tu nchini Tanzania, bali barani Afrika na duniani kwa ujumla,” amesema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Access Bank Group, Protase Ishengoma.
Mageuzi ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya nchini yameongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi, yamechochea kuimarika kwa biashara na kuvutia uwekezaji, yameboresha huduma za kijamii (afya, maji, elimu), kuimarisha amani, utulivu na demokrasia nchini, pamoja na kuongeza uwezo wa serikali kutekeleza miradi ya kimkakati ambayo inaboresha maisha ya wananchi.