Kazi ya Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kulinda amani ya nchi yetu imeendelea kutuletea matunda na heshima ambapo Tanzania imetajwa kuwa nchi yenye amani zaidi Afrika Mashariki kwa mujibu wa ripoti ya Global Peace Index ya mwaka 2025.
Amani ni msingi wa maendeleo yoyote ambayo jamii au taifa linalenga kuyafikia iwe kiuchumi, kijamii na kisiasa. Tanzania kutajwa miongoni mwa nchi zenye amani zaidi kunaendelea kuitangaza sifa njema kimataifa na hivyo kuifanya kuaminia na kuvutia biashara, uwekezaji na watalii zaidi, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akitoa hotuba ya kuhitimisha shunguli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais alisema nchi pamoja na wananchi wake wapo salama kutokana na kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya dola. Aidha, uimara huo umetokana na serikali kuvipatia vifaa vya kisasa, mafunzo, kuboresha maslahi pamoja na kuajiri watumishi wapya hivyo kuviongezea uwezo wa kutekeleza majukumu yake.
Ripoti hiyo ambayo imehusisha nchi 163 duniani imetumia vigezo 23 kupima amani ya nchi ikiwemo ulinzi na usalama wa jamii na kiwango cha migogoro ya kitaifa na kimataifa na matumizi. Tanzania imeshika nafasi ya kwanza ikiwafuatiwa na Rwanda, Uganda, Kenya, Burundi, Somali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini.