Kwa mara nyingine tena Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya makubwa na kuweka rekodi katika kuwatumikia wananchi. Rekodi hii mpya ni ya Gawio la Serikali ambapo kwa mwaka 2024/25 (hadi Juni 10, 2025) lilifikia TZS trilioni 1.028, kiwango cha juu zaidi katika historia ya nchi yetu.
Gawio hilo ambalo ni ongezeko ya asilimia 34 ikilinganishwa na TZS bilioni 767 zilipokelewa mwaka 2023/24 ni matokeo ya mabadiliko ya Mheshimiwa Rais, chini ya Falsafa ya 4R. Awamu ya Sita imefanya maboresho makubwa ya kisera, kisheria na kikanuni yaliyochagia kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, na hivyo mashirika hayo yakapata faida.
Aidha, kutokana na mabadiliko hayo, taasisi zilizotoa gawio hadi tarehe ya kupokea ziliongezeka kwa asilimia 47 toka taasisi 145 mwaka 2024 hadi taasisi 213 mwaka 2025, ikiwa ni kati ya taasisi/mashirika 309 ambayo serikali inamiliki/inaumiliki.
Akipokea gawio hilo, Mheshimiwa Rais aliwaeleza viongozi wa mashirika hayo kuwa gawio sio fadhila, bali ni wajibu kutokana na uwekezaji wa serikali. Hata hivyo, amewataka kutoyakamua mashirika ili nao waonekane wametoa gawio, badala yake watoe kwa mujibu wa sheria na kulingana na faida waliyopata.
Amesema kuwa lengo lake ni kuona mashirika yanachangia angalau asilimia 10 ya mapato yasiyo ya kodi kwa Serikali, ingawa sheria inataka yachangie asilimia 15. Alitumia wasaa huo kusisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza uchumi akisema kuwa “sekta binafsi ni kiungo muhimu katika safari ya mageuzi ya sekta ya umma na kwamba popote uhitaji utakapokuwepo, watashirikiana nao.