Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi kutosubiri amani ivunjwe ndipo wachukue hatua, badala yake wadhibiti viashiria vya uvunjifu wa amani, hasa wakati huu ambapo nchi inajiandaa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
“Niwatake mjipange vilivyo kuhakikisha mnaendelea kudhibiti viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani. Tusisubiri amani ivunjwe,” amesema Mheshimiwa Rais ambapo yeye kwa dhamana aliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ndiye mlinzi namba moja wa amani ya nchi.
Akizungumza katika sherehe za kufunga kozi ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi, mbali na suala la amani Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo mengine kwa jeshi hilo ili kuimarisha ari na ufanisi katika ulinzi wa raia na mali zao, ikiwemo kuzingatia maadili kwa kila askari kumheshimu mwenzake na kuepuka vitendo visiyokubali kama vile rushwa.
Maagizo mengine ni pamoja na kuzingatia haki, na kwamba askari hatakiwi kumwogopa mtu yeyote lakini hatakiwi kumwonea yeyote. Pia, amehimiza mafunzo ya utayari ambayo yanaendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, kuimarisha matumizi ya teknolojia, matahali kusomana kwa mifumo, kudhibiti dawa za kulevya na kujenga uhusiano na ushirikiano mwema na jamii pamoja na vyombo vingine vya dola vya nje ya nchi, hasa katika kudhibiti uhalifu unaovuka mipaka.
Aidha, amewataka wahitimu hao kuzingatia viapo vyao vya kazi, kuepuka vitendo vya rushwa na kuwa kielelezo cha mabadiliko chanya na maboresho ya kiutendaji kwenye maeneo yao ya kazi.