DP World yaongeza mapato Bandari ya Dar kwa zaidi ya TZS trilioni 1

Falsafa ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reform, and Rebuild) ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuleta mageuzi katika sekta mbalimbali zinazogusa maisha ya Watanzania na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchini.

Moja ya sekta hizo ni uchukuzi, ambapo Mageuzi (Reform) yaliyofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuingia ubia na Kampuni za DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL) katika kuendeleza na kuendesha baadhi ya maeneo ya bandari hiyo yameendelea kuleta matokeo, ikiwemo kuongeza mapato.

Kati ya Julai, 2024 hadi Februari 2025, mapato yatokanayo na Kodi ya Forodha kutoka bandarini yanayokusanywa kutokana na shughuli za kibandari yamefikia TZS trilioni 8.26, ambalo ni ongezeko la TZS trillion 1.18 ikilinganishwa na makusanyo ya TZS trilioni 7.08 yaliyokusanywa kipindi kama hicho kwa mwaka 2023/24.

Mafanikio hayo yametokana na wawekezaji hao kuwezesha upatikanaji wa vifaa na mitambo ya kisasa na mifumo ya TEHAMA inayoendelea kuleta ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za kibandari, hasa kuondoa msongamano wa mizigo na foleni za meli, hali inayochochea wafanyabiashara zaidi kuchagua kutumia bandari hiyo, hivyo kuongeza mapato.

Lengo la Mheshimiwa Rais Samia kushirikisha sekta binafsi ni kuongeza tija katika utendaji wa bandari nchini ili kuziwezesha zichangie zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu na maendeleo ya wananchi kwa ujumla kwa kuwafanya wanufaike na rasilimali za nchi yao.