Mheshimiwa Rais Samia Suluhu yupo nchini Korea ambapo amekamilisha ziara rasmi na sasa anaendelea na ziara ya kikazi hadi Juni 6 mwaka huu, ambapo hadi sasa Tanzania imeendelea kunufaika na ziara hiyo kufuatia kusainiwa kwa mkataba, tamko na hati za makubaliano ambazo zitaimarisha uhusiano uliopo na kufungua fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.
Kufuatia kusainiwa kwa makubaliano hayo, kumekuwa na upotoshaji mitandaoni ambapo moja ya vyombo vya habari kimeeleza kuwa Tanzania imepokea mkopo toka Jamhuri ya Korea na kutoa sehemu ya bahari na madini.
Balozi wa Tanzania nchini Korea, Togolani Mavura amekanusha habari hiyo akieleza kuwa Tanzania haijasaini mkataba wowote na Korea unaohusu bahari wala madini katika ziara ya Mheshimiwa Rais Samia, na kwamba katika ziara hiyo, Mheshimiwa Rais ameshuhudia utiwaji saini wa mkataba mmoja wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za kimarekani bilioni 2.5 kwa ajili ya miradi ya miundombinu.
Mbali na mkataba huo, Mheshimiwa Rais alishuhudia utiwaji saini wa hati za makubaliano (Memorandum of Understanding-MOU) mbili za ushirikiano katika sekta za uchumi wa buluu na madini ya kimkakati pamoja na Tamko la Utayari wa Kuanza Majadiliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (Joint Statement on the launch of Negotiation on Economic Partnership Agreement-EPA).
Amesisitiza kuwa Tanzania haijagawa chochote kubadilishana na mkopo nafuu kutoka Korea kama ilivyoandika, kwani inapata mkopo wa masharti nafuu kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo (EDCF) kwa mara ya tatu. Mara ya kwanza dola za kimarekani milioni 733 (2014-2020); mara ya pili dola bilioni 1 (2021-2025) na huu mkopo wa tatu ni dola bilioni 2.5 (2024-2028).
Aidha, ameweka wazi kuwa Tanzania ni moja ya nchi 59 zilizoko barani Afrika, Asia na Ulaya zinazofaidika na mkopo wa aina hii kutoka EDCF.
Mkopo ambao Tanzania imeupata, tofauti na ilivyopotoshwa na chomho hicho, ni mkopo wa masharti nafuu na una riba ya asilimia 0.01, unalipwa kwa miaka 40, na una fungate (grace period) ya miaka 25, yaani inaanza kulipa baada ya mwaka wa 26 na sio miaka mitano kama ilivyopotoshwa.