Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) limeipongeza serikali ya Tanzania kwa kuimarisha utulivu wa kiuchumi wakati ambapo dunia ilikuwa inapitia changamoto mbalimbali ikiwemo janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19), vita vya Urusi na Ukraine na mabadiliko ya tabianchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Bo Li baada ya kumaliza ziara yake nchini ambapo amesema “jitihada za haraka za serikali ya Tanzania zilisaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kulinda uchumi dhidi ya athari za vita nchini Ukraine.”
Licha ya mafanikio hiyo, taasisi hiyo imeihimiza Tanzania kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ambayo yatakuza uwezo wa Serikali katika kugharamia huduma za kijamii na kuongeza uwekezaji katika elimu, afya, maji na sekta nyingine muhimu.
Li akizungumza na wawakilishi wa sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wengine wa maendeleo ameeleza kuvutiwa sana na nguvu na uhai wa uchumi wa Tanzania.
Tanzania ni moja ya nchi chache barani Afrika zenye kiwango cha chini zaidi cha mfumuko wa bei ambapo kwa miezi sita mfululizo umekuwa ukishuka kutoka asilimia 4.9 Januari hadi asilimia 3.6 Juni mwaka huu.