Hatua ya Bunge la Tanzania kupitisha azimio la kuridhia ushirikiano kati ya Tanzania na Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika uendelezaji na uboreshaji utendaji kazi wa bandari Tanzania ni hatua nyingine kubwa katika mkakati wa Tanzania kuelekea kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji Afrika Mashariki na Kati ndani ya muongo mmoja ujao.
Kupitishwa kwa azimio hilo kunaipa nafasi Tanzania kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Dubai kupitia Kampuni ya DP World kuanza majadiliano yanayolenga kuangazia namna ya kushirikiana ili kuongeza ufanisi wa bandari nchini, hasa Bandari ya Dar es Salaam ambayo imekuwa lango la kibiashara kwa nchi za Afrika ya Mashariki, Kati na Kusini wa Afrika.
Kufanikiwa kwa ushirikiano baina ya Serikali hizi mbili kutatimiza ndoto ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ya kuongeza mapato ya bandari kutoka TZS trilioni 7.7 za sasa hadi TZS trilioni 26 ndani ya muongo mmoja, ambayo yataweza kufadhili shughuli za kijamii na kimaendeleo nchini, hivyo kupunguza utegemezi kwa washirika wa maendeleo, jambo ambalo ni msingi katika kudhihirisha Uhuru wa nchi kwenye kupanga na kuamua mambo yake.
Mafanikio mengine ambayo Tanzania itayapata ni kuongezeka kwa ajira kutoka nafasi 28,990 za sasa hadi ajira 71,907, kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 hadi saa 24, kupunguza muda wa ushushaji makontena kutoka siku 4.5 hadi siku 2, kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka saa 12 hadi saa 1, kupunguza gharama ya usafirishaji mizigo kutoka nje ya nchi kwenda nchi jirani kwa asilimia 50, pamoja na kuongeza shehena ya mizigo kutoka tani milioni 18 hadi tani milioni 47.
Mbali na manufaa hayo, uendelezaji wa bandari pia utachochea ukuaji wa sekta nyingine kama uvuvi, kilimo, ufugaji, viwanda na biashara, usafirishaji (anga, reli, barabara), kiimarisha diplomasia pamoja na Watanzania kunufaika na teknolojia na ujuzi wa uendeshaji wa bandari kisasa.
Ili kuendeleza uwazi na uwajibika, Serikali chini ya Rais Samia imeahidi kuwa mikataba itakayoandaliwa itaweka bayana kipindi cha utekelezaji wake na ukomo, muda wa marejeo na viashiria muhimu vya ufanisi wa kiutendaji, na uandaaji wake utafanywa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.