‘Champion’ wa mageuzi ya demokrasia, ndiyo sifa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris aliyompa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na mageuzi ya kisiasa aliyofanya nchini ikiwa ni pamoja na kuruhusu mikutano ya hadhara, kukutana na viongozi wa vyama vya siasa na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari.
Kutokana na uongozi bora wa Rais Samia, Marekani na Tanzania zimekubaliana kupanua ushirikiano ambao utawezesha upatikanaji wa dola za Kimarekani milioni 500 (TZS trilioni 1.2) kugharamia uletaji wa bidhaa na huduma nchini Tanzania katika sekta za usafirishaji, nishati salama, teknolojia ya kidijitali na miundombinu.
Aidha, katika muktadha huo wa kukuza uchumi amesema kazi ya ujenzi wa kiwanda cha kwanza na cha aina yake Afrika kitakachotumika kuchakata madini yanayotengeneza betri za magari ya umeme ambayo yatakuwa yanatumika duniani kote ikiwepo Marekani inandelea na uzalishaji utaanza mwaka 2026.
Kuongezeka kwa fursa hizi kutazalisha ajira kwa maelfu ya Watanzania, na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya kiuchumi Afrika na duniani.
Wakati huo huo, Kamala amempongeza Rais Samia kwa namna miaka miwili ya uongozi wake imewezesha kumwinua mwanamke kiuchumi, akisisitiza kuwa mwanamke akiinuliwa kiuchumi, basi familia na jamii nzima inanufaika.