Maendeleo ya Watanzania na maendeleo ya nchi yanategemea sana upatikanaji wa nishati ya uhakika, na kwa kulitambua hilo, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu katika miaka yake miwili ya uongozi ameendelea kuimarisha sekta hiyo ambayo imefungua zaidi fursa za kiuchumi kwa wananchi, ushuhuda wa karibuni ukiwa ni wananchi wa Kigoma walioanza kunufaika na umeme wa gridi ya Taifa ambao ni wa uhakika zaidi kuliko uliokuwa ukizalishwa kwa majenereta.
Katika muktadha huo huo wa kuwawezesha wananchi, Serikali imesaini mikataba ya utekelezaji wa miradi mikubwa mitatu ya kupelekea umeme zaidi vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), miradi ambayo itagusa sekta za kilimo, afya, maji, viwanda vidogo na madini.
Mradi wa kwanza (Ujazilizi 2B) ambao utafikisha umeme katika vitongoji 1,522 ambao utaunganisha umeme kwa wananchi zaidi ya 88,000. Mradi wa pili unapeleka umeme kwenye migodi na maeneo yenye shughuli za kilimo 336 yaliyopo katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Mradi huu utawapunguzia gharama (fedha na muda) za uchimbaji madini wachimbaji wadogo, utazalisha ajira zaidi, utawawezesha kutumia teknolojia ya kisasa, utachochea ukuaji wa sekta ya madini pamoja na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa.
Aidha, kwa kufikisha umeme katika maeneo yenye shughuli za kilimo kunaendana na lengo la Serikali la kuifanya Tanzania kuwa kapu la chakula kwa Afrika, kwa kuvutia vijana kufanya kilimo cha kibiashara. Umeme utasaidia katika umwagiliaji na uongezaji thamani wa mazao.
Mradi wa tatu unahusisha kupeleka umeme katika vituo vya afya 63 na pampu za maji 333 vijijini katika mikoa 25. Kufika kwa nishati kwenye maeneo hayo kutaboresha utoaji huduma za afya, mathalani nyakati za usiku, kutapunguza vifo vya mama na mtoto, na kuwezesha upatikanaji huduma nyinginezo zinazohitaji umeme.
Wakati huo huo, uwepo wa umeme unaosukuma maji katika pampu utahakikisha vijiji vinakuwa na maji ya uhakika, hatua ambayo itakuza usafi na kupambana na magonjwa ya mlipuko, lakini pia itapunguza muda wa wananchi kufuata maji, hivyo kushiriki katika shughuli nyigine za kimaendeleo.
Kwa miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia, REA imesaini mikataba ya TZS trilioni 2.2, ambapo kati ya fedha hizo, TZS trilioni 1.7 ni za Serikali, hatua inayodhihirisha dhamira ya Rais kufikisha umeme kwa wananchi. Kutokana na miradi inayoendelea, vijiji vyote vya Tanzania vitafikiwa na nishati ya umeme ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023.