Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema sekta ya kilimo nchini inatarajiwa kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 ikilinganisha na ukuaji wa sasa wa takribani asilimia 3.6.
Akizungumza kwenye mdahalo wa ‘Food Action Partnership: Investing in Greater Resilience’ nchini Uswisi amesema Tanzania imetengeneza fursa za kitaifa kwa ajili ya mabadiliko ya mfumo wa chakula unaotarajia kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha maisha ya watu na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Katika kudhibiti mfumo endelevu wa chakula nchini, Rais Samia amesema jitihada kadhaa zimefanyika, ikiwemo kuanzisha mradi kwa ajili ya vijana huku wakiendelea kuimarisha ukuaji wa shoroba za kilimo pamoja na kuongeza bajeti ya kilimo mara 4 ukilinganisha na ile iliyopita.
Serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza miradi na mafunzo mbalimbali ya kilimo kwa vijana ili kuongeza tija kwenye kilimo na kuwezesha vijana kushiriki kwenye uchumi wa Tanzania ambapo lengo ni kuzalisha ajira milioni 1 ifikapo mwaka 2025.
Mdahalo huo uliohudhuriwa na zaidi ya viongozi 50 kutoka Afrika, Asia, Ulaya na Marekani mbali na Rais Samia wachangiaji wengine walikuwa Rais Gustavo Petro wa Colombia, Tran Hong Ha, Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam na Alvaro Lario, Rais wa Wakfu wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Roma.