Mkakati wa kibiashara wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan unaendelea kuwa na matokeo chanya katika dira ya Serikali ya kukuza uchumi ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa thamani ya miradi ya uwekezaji imeongezaka karibu mara tatu ndani ya kipindi cha miezi mitano.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetoa taarifa inayoonesha kuwa kimesajili miradi 132 yenye thamani ya TZS trilioni 7 kati ya Julai hadi Novemba mwaka huu ambapo sekta ya viwanda, usafirishaji na utalii ndizo zimeongoza kwa uwekezaji. Usajili huo ni ongezeko la miradi 24 kutoka miradi 108 yenye thamani ya TZS trilioni 2.06 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2021.
Miradi hiyo ambayo imeongezeka kwa idadi na thamani, itatoa ajira 21,297 ambazo ni ongezeko la asilimia 57 kutoka ajira 13,578 za mwaka jana ni matokeo ya Diplomasia ya Uchumi ambayo Rais amekuwa akiitekeleza kwa vitendo.
Rais Samia ameendelea kuimarisha mahusiano ya kibiashara ndani ya nchi, kikanda na kimataifa katika ziara mbalimbali anazofanya ambazo huambatana na wafanyabiashara wa ndani ambao hupata fursa ya kuzungumza na wafanyabiashara wa nje, lakini pia huwezesha Tanzania na nchi nyingine kuingia makubaliano ya kibiashara na uwekezaji.
Tangu aingie madarakani Rais amefanikiwa kurejesha imani ya wawekezaji ambao sasa wanaamani ya kuja na kuwekeza nchini. Katika muda huo ametatua changamoto mbalimbali za kibiashara kama vile kupunguza muda wa kupata vibali vya uwekezaji, kurekebisha mifumo ya kikodi, kuondoa ukiritimba wa vibali vya kazi na kuwepo kwa maeneo maalum ya uwekezaji.