“Si wakati wakati wote ni wa kupongezana na si wakati wote ni wa kupingana. Kwenye kujenga Tanzania bora natamani kujenga jamii yenye maridhiano na maelewano. Natamani kujenga umoja pasipo kujali tofauti zetu za kisiasa, kidini, kikabila na nyingine zote.”
Hayo ni maneno ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika barua yake aliyoitoa Tanzania ikiadhimisha miaka 30 tangu kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi, ambapo alieleza azma yake ya kujenga jamii inayopata haki sawa mbele ya sheria, isiyobaguana na inayotoa fursa sawa za kiuchumi kwa wote.
Katika kufanikisha nia hiyo, Rais ametimiza kiu ya muda mrefu ya vyama vya upinzani kwanza kwa kukutana na kuzungumza na wanasiasa wa upinzani akiwemo viongozi wa CHADEMA, CUF na ACT-Wazalendo, mazungumzo ambayo yameendelea kujenga imani miongoni mwa viongozi hao kuhusu nia thabiti ya Rais kujenga umoja wa kitaifa.
Aidha, katika kutekeleza matakwa na viongozi wa vyama vya upinzani ambayo ni pamoja na kufufuliwa kwa mchakato wa katiba mpya na kuundwa tume huru ya uchaguzi, Rais aliunda kikosi kazi kilichojumuisha wawakilishi kutoka vyama vya upinzani, na tayari kimewasilisha mapendekezo serikali juu ya namna ya kuyafikia matamanio hayo.
“Mama Samia amekuwa Rais wa kwanza kwenye nchi yetu baada ya ujio wa pili wa vyama vingi mwaka [19]92 kusimama hadharani, na nilisimama naye Ikulu, tukazungumza na vyombo vya habari mimi na yeye, kwamba tufanye nini kila mmoja […] tuondoe maumivu yaliyopo katika Taifa hili,” alisema Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe Machi 2022.
Uamuzi wa Mbowe kusimama kwenye maridhiano umeungwa mkono na viongozi wa CHADEMA ambapo aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi amesema kwa sababu njia za maandamano walizowahi kujaribu huko nyuma hazikufanikiwa, basi, sasa njia ya kuelekea ni maridhiano.
Kwa upande wake kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema “hakuna njia yoyote ya kuifanya nchi yetu iweze kwenda mbele isipokuwa njia hii ambayo [Rais Dkt. Samia Suluhu] unaipita ya kujenga maridhiano ya kitaifa.”
Kufikia maridhiano, Rais pia anahakikisha haki inapatikana ambapo katika barua yake alisema anaamini “maridhiano hayawezi kupatikana penye ubaguzi na pale ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia.”