Tanzania imeongoza Afrika Mashariki kwa kasi kubwa ya ongezeko la thamani ya uwekezaji kutoka nje ya nchi ambapo imeongezeka kwa asilimia 28.3 kutoka dola za Marekanili bilioni 1.34 (TZS trilioni 3.5) mwaka 2023 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1.72 (TZS trilioni 4.4) mwaka 2024.
Aidha, kasi hiyo kubwa ya ongezeko la uwekezaji imeifanya Tanzania kushika namba 11 Afrika kwa kiwango kikubwa cha uwekezaji toka nje, na nafasi ya 13 kwa ukuaji wa thamani ya uwekezaji. Pia, umeiwezesha Tanzania kuvuka kiwango cha asilimia 12 cha ukuaji wa uwekezaji kilichowekwa kwa nchi za Afrika Mashariki na bara la Afrika.
Ukuaji huo ni matokeo ya kazi kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ameendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi pamoja na kutangaza fursa zilizopo kimataifa na hivyo kupelekea kuongeza kwa miradi ya uwekezaji.
Mwaka 2024 Tanzania iliweka rekodi kwa kusajili miradi 901 ya uwekezaji kutoka miradi 526 mwaka 2023 ambapo maelfu ya wananchi watanufaika na ajira, na miradi hii itachagiza ukuaji wa sekta nyingine kama nishati, maji, mawasiliano, usafirisha, huduma na uzalishaji.