MAMA aweka rekodi kubwa nne makusanyo ya kodi kwa mwaka 2024/25

Mwaka 2024/25 umekuwa mwaka wa rekodi kwenye ukusanyaji wa mapato nchini, ukusanyaji wa mapato wa TZS shilingi 32.26, sawa na ufanisi wa asilimia 103.9, umeiwezesha Serikali ya Awamu ya Sita kuweka rekodi kubwa nne.

Rekodi zilizoweka ni kuvuka kwa lengo la mwaka la makusanyo ya kodi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2015/16. Rekodi ya pili ni kuvuka lengo la makusanyo ya kila mwezi kwa miezi 12 mfululizo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka 1996.

Rekodi ya tatu ni kuongezeka kwa wastani wa makusanyo ya kila mwezi hadi shilingi trilioni 2.69, ambacho ni kiwango cha juu zaidi katika historia ya TRA. Aidha, rekodi ya nne ni kufanikisha makusanyo ya juu zaidi kwa mwezi mmoja ambapo shilingi trilioni 3.58 zilikusanywa Desemba 2024.

Matokeo haya yamechangiwa na kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Miongoni mwa aliyofanya ni kurekebisha sheria na kanuni 66 pamoja na kufuta au kupunguza kodi, ada na tozo 383 ili kuondoa adha kwa wafanyabiashara.

Hatua hizo zimeongeza ushirikiano mzuri kati ya TRA na walipakodi jambo ambalo limeongeza utayari wa wananchi kulipa kodi, kukua kwa shughuli za biashara na uwekezaji, kuimarika kwa ufanisi wa TRA katika kushughulikia masuala ya wateja, hasa kutokana na mamlaka hiyo kuongezewa watumishi.