Katika hotuba ya zaidi ya saa tatu kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Suluhu Hassan ametumia zaidi ya dakika nane kuwaeleza wananchi kuhusu Deni la Serikali kufuatia uwepo wa upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu juu ya sababu halisi ya kuongezeka kwa deni hilo kufikia TZS trilioni 107.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Rais amesema moja ya sababu ni kupokewa kwa fedha za mikopo mipya na ya zamani ambayo mikataba yake ilisainiwa wakati wa awamu zilizopita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“… mkopo unaweza kusainiwa leo lakini fedha husika zikaanza kupokelewa baada maandalizi ya mradi kukamilika na mradi kuanza. Hivyo, ili mkopo huo uingie kwenye deni la serikali ni lazima serikali iwe imepokea fedha hizo,” amesema hayo na kuongeza kuwa Awamu ya Sita imepokea TZS trilioni 11.3 ikiwa mikopo ya awamu zilizopita.
Aidha, sababu nyingine ni kuimarika kwa dola ya Marekani dhidi ya shilingi ya Tanzania ambapo kutokana na utofauti wa viwango vya kubadili fedha, deni hilo limeongezeka kwa TZS trilioni 3.9. Licha ya kuwa kwa upande wa dola linabakia kiwango kile kile, lakini linapotajwa kwa shilingi ya Tanzania lazima lionekane limeongezeka kutokana na kushuka thamani kwa shilingi.
“Hatua ya kushuka thamani kwa shilingi dhidi ya dola ya Marekani isichukuliwe kama ni hatua hasi, bali ilikuwa ni hatua muhimu ya kukabiliana na mtikisiko wa uchumi wa dunia,” amesisitiza Mheshimiwa Rais.
Kwa upande mwingine, ongezeko la Deni la Serikali la Ndani kumetokana na mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kulipa madeni ya ndani yaliyoiva. Pia, ongezeko limetokana na serikali kutambua madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa serikali kupitia hati fungani maalum isiyo taslimu yenye thamani ya TZS trilioni 2.6.
“Lengo la hatua hizi ni kunusu mifuko ya hifadhi ya jamii, lakini pia wastaafu wetu waliotumikia taifa wanapata mafao kwa wakati,” ameeleza.
Mheshimiwa Rais ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kusimamia deni la serikali liwe himilivu, na pia itaongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa mikopo katika ugharamiaji wa bajeti za nchi.