MAMA aboresha Sera ya Mambo ya Nje ili kukuza Diplomasia ya Uchumi na kulinda utamaduni wetu

AKIAHIDI, ANATIMIZA. Hayo ndiyo maneno mawili yanayoweza kutumika kueleza tukio la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzindua Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 (Toleo la Mwaka 2024), ambayo ni ahadi aliyoitoa Aprili 2021 wakati akihutubia bunge, mwenzi mmoja baada ya kuingia madarakani. Akizungumza bungeni alisema kuwa serikali itaifanyia maboresho sera hiyo ili iendane na mabadiliko ambayo yametokea ndani na nje ya nchi katika sekta mbalimbali.

Ikiwa ni miaka 24 tangu kupitishwa kwa sera hiyo, leo Mei 19, 2025 Mheshimiwa Rais amezindua toleo hilo ambalo limejikita katika Diplomasia ya Uchumi likilenga kulisukuma Taifa mbele na kuimarisha ushiriki na ushindani katika siasa na maendeleo ya kimataifa, kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania kupitia diplomasia makini na shirikishi.

Toleo la mwaka 2024 limeleta maboresho mbalimbali ambayo ni pamoja na kuongeza msingi mmoja (wa nane) katika Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Msingi huo ni kulinda na kuendeleza maadili, mila na utamaduni wa Mtanzania ikiwemo kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili, hatua ambayo inalenga kukabiliana na uvamizi mkubwa wa utamaduni na ustaarabu unaoendelea.

Aidha, mambo mengine manne yaliyoongezwa ni, moja, kuimarisha Diplomasia ya Uchumi kwa kuvutia uwekezaji wa mitaji mikubwa, kutumia vizuri fursa ya kijografia tuliyojaliwa na kufaidika na soko huru la biashara Afrika. Pili, ni matumizi ya lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya kujenga ushawishi ili kupanua masoko ndani na nje ya Afrika. Tatu, kukuza ushiriki wa Diaspora katika kukuza uchumi wao binafsi na uchumi wa taifa, na nne ni kuangalia fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi ikiwemo uchumi wa buluu ili kuchochea ukuaji wa kiuchumi.

Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wote walioshiriki kuandaa sera hiyo, hasa wananchi waliotoa maoni akisema kuwa “mmeshiriki katika kujenga hatma ya nchi yenu na mmeweka alama isiyofutika.”