Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali nchini ambapo katika sekta ya maji, ndani ya kipindi cha miaka minne amekamilisha miradi ya maji zaidi ya 2,331 mijini na vijijini ambayo imefikisha maji kwa mamilioni ya wananchi.
Kutokana na ufanisi huo asilimia 83 ya wakazi wote wa vijijini wanapata maji safi na salama ikiwa ni ongezeko toka asilimia 72.3 alizokuta wakati anaingia madarakani Machi 2021. Aidha, kwa sasa asilimia 91.6 ya wananchi wa mijini wanapata huduma ya maji safi na salama ikilinganishwa na wastani wa asilimia 86 aliyoikuta.
Mafanikio haya yanakaribia lengo lililoanishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025) ambayo inaielekeza serikali kuongeza kasi ya usambazaji majisafi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya asilimia 85 vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini, kwa upande wa Tanzania Bara, ifikapo Desemba 2025.
Ili kuhakikisha lengo la ilani, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji 1,544. Hatua hii inadhihirisha dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais kufikisha maji kwa kila mwananchi popote alipo akitambua kuwa maji ni uhai, maendeleo na usalama kwa wananchi.