Ni furaha furi furi kama sio furaha bojo bojo kwa watumishi wa umma na Watanzania kwa ujumla baada ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza nyongeza ya kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 35.1. Kutokana na nyongeza hiyo, kima cha chini kuanzia Julai 1, 2025 kitakuwa TZS 500,000 toka kiwango cha TZS 370,000 cha sasa.
Mheshimiwa Rais ametangaza neema hiyo katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Dunia (Mei Mosi) ambayo kitaifa imefanyika mkoani Singida ikiwa na kaulimbiu isemayo, “Uchaguzi Mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi wote, sote tushiriki.”
Amesema nyongeza hiyo ni sehemu ya hatua ambazo serikali yake imeendelea kuchukua kuleta ustawi kwa wafanyakazi nchini, na kwamba uamuzi huo umewezeshwa na kasi ya ukuaji wa uchumi kupanda hadi kufikia 5.5% kwa mwaka, hali iliyochangiwa na wafanyakazi kujituma na kufanya kazi kwa bidii.
Kupitia mitandao ya kijamii wananchi wamefurahia nyongeza hiyo ambapo wameandika jumbe za kumpongeza. Baadhi ya jumbe hizo ni;
“Nakuamini na nakupenda sana mama maisha yangu yote sijawahi kupiga kura ila mwaka huu inshallah nna Imani kura yangu unayo ya kwanza kwenye maisha yangu,”- Hamoud Jimia.
“Ubarkiwe mama ikulu yako huna mpinzani hata kidgo,”- Kisila Legandy
“Safi mama Samia, wewe ndo unatudai na tunakuhakikishia lazima tukulipe,”- Julius Peter
“Kima cha chini cha mashahara kinapanda kutoka 300k mpaka 500k nomaa,”- Msaki.
Kuhusu sekta binafsi Mheshimiwa Rais amesema kuwa Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara inaendelea na tathmini kwa lengo la kuboresha viwango vya mishahara kwa sekta binafsi.
“Tutaendelea kuboresha mazingira ya wafanyakazi ikiwemo maslahi ya wafanyakazi kwa kadiri hali itakavyoruhusu… Ili tuweze kujenga vyema Taifa letu ni lazima tulinde amani na utulivu nchini,” amesisitiza Rais Dkt. Samia.