Serikali imetangaza wanafunzi wote 974,332 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2025 bila kusubiri machaguo kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita.
Kwa miaka kadhaa iliyopita ilizoeleka wanafunzi waliohitimu darasa la saba aidha kushindwa kujiunga au kujiunga na elimu ya sekondari kwa mafungu kutokana na sababu mbalimbali lakini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan suala hilo limefikia ukomo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI wanafunzi wote waliofaulu wataanza masomo kwa wakati mmoja ikiwa ni matokeo ya maandalizi ya mapema yaliyofanywa na Serikali ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2024 wanajiunga na elimu ya sekondari ifikapo Januari 13, 2025.
Miongoni mwa shughuli za maandalizi zilizofanyika ni kujenga na kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa, nyumba za walimu pamoja na uwepo wa madawati na walimu wa kutosha ikikukmbukwa kuwa serikali imetangaza ajira mpya za walimu 3,633 hivi karibuni.
Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wasichana ni 525,225 na wavulana ni 449,107.