Rais Samia akutana na viongozi wa Ngorongoro, kuunda Tume mbili

Jumapili, Desemba mosi, 2024 katika Ikulu ndogo ya Arusha, Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa na wa kimila wa jamii ya Kimaasai (Malaigwanani) wanaoishi eneo la Ngorongoro na maeneo ya jirani.

Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwepo kwa malalamiko dhidi ya baadhi ya maamuzi ya Serikali yanayohusu eneo la Ngorongoro.

Katika mazungumzo hayo Rais Dkt. Samia amesema ataunda Tume mbili ambapo moja itachunguza na kutoa mapendakezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro na nyingine itaangalia utekelezaji wa zoezi zima la uhamiaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Rais Dkt. Samia amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na jamii hiyo huku pia akisisitiza ulazima wa wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji miradi inayopita kwenye maeneo yao.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye Serikali inayowahudumia Watanzania wote. Hivyo, ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la  Ngorongoro.