December 2024
-
Serikali imetangaza wanafunzi wote 974,332 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2025 bila kusubiri machaguo kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita. Kwa miaka kadhaa iliyopita ilizoeleka wanafunzi waliohitimu darasa la saba aidha kushindwa kujiunga au kujiunga na elimu ya sekondari kwa mafungu kutokana na sababu mbalimbali lakini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan suala hilo limefikia ukomo. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI wanafunzi wote waliofaulu wataanza masomo kwa wakati mmoja ikiwa ni matokeo ya maandalizi ya mapema yaliyofanywa na Serikali ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2024 wanajiunga na elimu ya sekondari ifikapo Januari 13, 2025. Miongoni mwa shughuli za maandalizi zilizofanyika ni kujenga na kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa, nyumba za walimu pamoja na uwepo wa madawati na walimu wa kutosha ikikukmbukwa kuwa serikali imetangaza ajira mpya za walimu 3,633 hivi karibuni. Kati ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wasichana ni 525,225 na wavulana ni 449,107. Read More
-
Jumapili, Desemba mosi, 2024 katika Ikulu ndogo ya Arusha, Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa na wa kimila wa jamii ya Kimaasai (Malaigwanani) wanaoishi eneo la Ngorongoro na maeneo ya jirani. Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwepo kwa malalamiko dhidi ya baadhi ya maamuzi ya Serikali yanayohusu eneo la Ngorongoro. Katika mazungumzo hayo Rais Dkt. Samia amesema ataunda Tume mbili ambapo moja itachunguza na kutoa mapendakezo kuhusu masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro na nyingine itaangalia utekelezaji wa zoezi zima la uhamiaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Rais Dkt. Samia amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na jamii hiyo huku pia akisisitiza ulazima wa wananchi kushirikishwa ipasavyo katika upangaji na utekelezaji miradi inayopita kwenye maeneo yao. Aidha, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi inayojivunia umoja wa kitaifa na yenye Serikali inayowahudumia Watanzania wote. Hivyo, ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kushughulikia changamoto zinazojitokeza ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya huduma za msingi za kijamii katika eneo la Ngorongoro. Read More