Kati ya mwezi Januari hadi Julai 2024 jumla ya ajira 607,475 zimezalishwa nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kufikia lengo la kuzalisha ajira milioni 1.2 kila mwaka.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma. Jitihada za kuhakikisha watanzania wanapata ajira zinaakisi lengo la kuzalisha ajira milioni nane kama ilivyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025.
Akizungumzia maeneo ambayo Serikali inayaangazia katika kuzalisha ajira ameeleza kuwa Serikali inatumia balozi zake kutafuta nafasi za kazi kwa watanzania kwenye maeneo yalipo balozi hizo. Vilevile ametaja njia nyingine kuwa ni kupitia taasisi za elimu, wizara na vyuo vikuu ambako baadhi ya watanzania wanapata ajira nje ya nchi, zikiwamo nafasi za utafiti na fursa kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Pia Naibu Waziri Katambi ameeleza kuwa Serikali tayari imeanza kutekeleza mpango maalumu kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) ili kubaini ajira zinazotangazwa mtandaoni na kuwafikia watanzania katika kanzidata, pia kuwasaidia kwa mafunzo ili kuhakikisha wanastahili kupata ajira hizo.