Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu hali ya uchumi kwa Mei 2024 imeonesha kuwa watalii wameendelea kumiminika nchini ambapo miezi ya Machi na Aprili ambayo ilitambulika huko nyuma kwa kuwa na idadi ndogo ya watalii (low season), kwa mwaka 2024 watalii wa kimataifa wameongezeka kwa asilimia 21.9 na asilimia 21.8 mtawalia ikilinganishwa na miezi kama hiyo mwaka jana.
Hali hii ambayo ni matokeo ya kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii nchini na duniani inaifanya sekta hiyo kuendelea kuwa chanzo kikubwa cha fedha za kigeni ambapo katika miezi hiyo utalii umeingiza dola za Marekani bilioni 3.58 kwa Machi na dola za Marekani bilioni 5.75 kwa Aprili kutoka dola za Marekani bilioni 2.7 na dola za Marekani bilioni 2.8, mtawaliwa kwa miezi kama hiyo mwaka jana 2023.
Mafanikio haya yametokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali pamoja na sekta binafsi ikiwemo kutangaza vivutio vya utalii nje ya nchi, huduma bora kwa wageni wanaofika kutalii nchini pamoja na kuimarisha huduma za usafiri, mathalani sekta ya anga.
Ripoti ya BoT inaunga mkono utafiti uliofanywa na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kwa robo ya Januari-Machi 2024, ambapo kwa ukuaji unaoendelea sasa wa sekta ya utalii, Tanzania ilishika nafasi ya kwanza Afrika na ya nne duniani kwa ongezeko kubwa la watalii ikilinganishwa na kabla ya UVIKO-19, yaani mwaka 2019.
Mafanikio na kuimarika kwa sekta ya utalii, pamoja na sekta nyinginezo kama madini, usafirishaji, kilimo kutaendelea kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kufikia asilimia 5.8 mwaka huu.