Mama Yuko Kazini: Miradi ya uwekezaji yaongezeka mara mbili robo ya kwanza ya 2024

Mikakati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kupitia Diplomasia ya Uchumi inazidi kuzaa matunda ambapo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili ongezeko la miradi ya uwekezaji kwa asilimia 111, kutoka miradi 100 Januari hadi Machi 2023 hadi miradi 211 kipindi kama hicho mwaka 2024.

Thamani ya uwekezaji huo imeongezeka kwa USD milioni 217.98 (TZS bilioni 566.75) kutoka USD bilioni 1.26 (TZS trilioni 3.26) katika robo ya kwanza ya mwaka 2023 hadi kufikia USD bilioni 1.48 (TZS trilioni 3.85) katika robo ya kwanza ya mwaka 2024.

Uwekezaji huu utawanufaisha maelfu ya wananchi ambapo idadi ya ajira imeongezeka kufikia 24,931 katika kipindi tajwa kwa mwaka 2024 kutoka ajira 17,016 zilizosajiliwa mwaka jana, sawa na ongezeko la asilimia 46.5.

Mafanikio haya ni matokeo ya hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwemo kuboresha Sheria ya Uwekezaji ambayo inatoa msamaha wa ushuru wa forodha wa asilimia 75, imepunguza kiwango cha mtaji wa uwekezaji kwa wazawa toka USD 100,000 hadi USD 500,000.

Mengine yaliyofanyika ni kuwa na kituo cha pamoja ambacho mwekezaji atapata huduma zote, kuwezesha usajili wa miradi kwa njia ya mtandao, kufuta au kupunguza ada na tozo, kurahisisha utoaji wa leseni pamoja na kufanya mikutano na wafanyabishara nje ya nchi, hasa kupitia ziara za Mheshimiwa Rais na maonesho mbalimbali, ambavyo vimeendelea kuitangaza nchi yetu na kuendelea kuimarika kwa amani na utulivu nchini.