Matokeo ya mageuzi ambayo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu anayasimamia kupitia falsafa yake ya 4R yanazidi kuonekana kupitia sekta mbalimbali ambapo utashi wake wa kisiasa umeendelea kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari.
Mei 3 ya kila mwaka dunia huadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ambavyo huchukuliwa kuwa ni mhimili wa nne wa dola, vikiwa na kazi ya kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi, kulinda maslahi ya wananchi, kuunganisha wananchi na kuchochea maendeleo.
Mwaka 2024 yamefanyika maadhimisho ya 31 tangu azimio la Windhoek, na maadhimisho ya nne tangu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ambapo uongozi wake umekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uhuru na hali ya kiuchumi wa vyombo vya habari.
Uthibitisho huo unaonekana kwenye ripoti ya Reporters Without Boarders (RWB) ambayo imeitaja Tanzania kuwa namba moja Afrika Mashariki kwa kulinda uhuru wa vyombo vya habari. Aidha, utafiti huo umeonesha Tanzania imepiga hatua kubwa duniani ikipanda toka nafasi ya 143 mwaka 2023 hadi nafasi ya 97 mwaka huu.
Utafiti huo umeangazia mambo mbalimbali yakiwemo misingi ya kisheria, hali ya kiuchumi, hali ya kisiasa, usalama wa wanahabari na dhana ya kijamii na kitamaduni.
Haya ni matokeo ya dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari ambapo alipoingia madarakani alifungulia magazeti na televisheni za mitandaoni zilizokuwa zimefungiwa, ameunda kamati ambayo imekamilisha kazi ya kuangalia hali ya kiuchumi ya vyombo vya habari pamoja na kuruhusu taasisi za Serikali kupeleka matangazo kwenye vyombo binafsi.
Mafanikio haya pia yamechangiwa na mabadiliko ya Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari 2016 na baadhi ya Kanuni za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) 2010, na mikakati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa elimu sheria za utangazaji na kimtandao hivyo kuviwezesha vyombo vya habari kuzingatia sheria.
Mwaka 2022 Mheshimiwa Rais aliweka rekodi ya kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika jijini Arusha, hatua ambayo ilidhihirisha dhamira yake ya kukuza sekta hiyo ambayo pia imetoa ajira kwa maelfu ya vijana pamoja na kuonesha namna anavyotambua mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo wa Tanzania.