Kujua unakokwenda ni muhimu ili kuweza kufika, lakini njia ipi uitumie si tu ili ufike, bali ufike kwa wakati, ni muhimu zaidi.
Tanzania inalenga kujenga uchumi ambao pamoja na mambo mengine utapunguza kiwango cha umasikini kwa mamilioni ya wananchi, ili kufanikisha hilo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameamua kuitumia sekta ya kilimo ambayo inagusa maisha ya Watanzania saba katika kila Watanzania 10.
Takwimu zinaunga mkono uamuzi wake kuwa kilimo kinachangia asilimia 26 ya Pato la Taifa, kinatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 62 ya wananchi, kinachangia dola bilioni 2.3 kwa mwaka, hutoa malighafi za kiwandani kwa asilimia 65 na kinahakikisha usalama wa chakula nchini kwa asilimia 100. Hili ni wazi kuwa mageuzi ya kweli katika maisha ya wananchi ni lazima yahusishe kilimo, siri ambayo MAMA anaijua.
Ni vigumu kueleza yote yaliyofanyika katika miaka mitatu ya MAMA madarakani kwani ni mengi mno. Baadhi ya mambo hayo ni bajeti ya kilimo imeongezwa zaidi ya mara tatu kutoka TZS bilioni 294 mwaka 2021/22 hadi TZS bilioni 970 mwaka 2023/24, ongezeko ambalo ni msingi wa mageuzi yote kwenye sekta hiyo.
Ongezeko hilo limepelekea mafanikio makubwa katika uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia ambapo matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 363,599 hadi tani 580,628 kutokana na mpango wa mbolea ya ruzuku. Matumizi ya mbolea yameongeza uzalishaji wa mazao ulioiwezesha nchi kuongeza mauzo ya nje takribani mara mbili kutoka TZS trilioni 3 hadi TZS trilioni 5.7.
Mageuzi yaliyofanyika yamemfikia mkulima katika ngazi ya kijiji kupitia vifaa vilivyotolewa kwa maafisa ugani wa halmashauri 166 zikiwemo pikipiki 5,889, vishkwambi 805, seti za vifaa vya kupimia udogo 143 ambavyo vimemwezesha mkulima kulima kisasa akijua atumie mbegu gani na mbolea gani kwenye aina fulani ya udongo.
Kama hayo hayatoshi kuondoa kilimo cha mazoea tena cha msimu, MAMA amewekeza katika kilimo umwagiliaji kwa kuongeza bajeti ya umwagiliaji kwa takribani mara nane kutoka TZS bilioni 46.5 hadi TZS bilioni 361.5. Uwekezaji umeongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 822,000 kutoka hekta 727,281 ambapo lengo ni kufikia hekta milioni 1.2 ifikapo mwaka 2025.
Aidha, MAMA amefufua Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na kuipa mtaji wa jumla ya shilingi bilioni 116 kwa ajili ya kufanya biashara ya mbolea nchini, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu (asilimia 4.5) kwa wakulima, hasa wanawake na vijana, ambao wananufaika na mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) unalenga kuwawezesha kufanya kilimo cha kisasa na cha kibiashara.
Mfanikio mengine ni kuanzishwa kwa kiwanda cha mbolea cha Itracom, kuanzishwa Benki ya Taifa ya Ushirika ili kuviwezesha vyama vya ushirika kupata mikopo, kupunguza riba ya mikopo ya kilimo hadi asilimia 9, kuandaa mikutano ya kimataifa na kushiriki kwenye maonesho ya kimataifa ambayo yameiwezesha nchi kupata masoko mapya ya mazao na wawekezaji.
Kwa uchache huu ni wazi kuwa MAMA ana dhamira ya dhati ya kumwinua Mtanzania kupitia kilimo, tena ikikumbuka kwamba sekta hii ni muhimu katika ukuaji wa sekta nyingine pamoja na kuendelea kutunza mazingira. Hatua hizi ambazo zimeanza kuleta matunda zinalenga kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.