Diplomasia ya Uchumi: Mheshimiwa Rais Samia avutia wafanyabiashara zaidi wa Norway kuwekeza Tanzania

Mwanadiplomasia namba moja wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameendelea kutekeleza kwa vitendo Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Diplomasia ya Uchumi, katika ziara zake nje ya nchi kwa kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini pamoja na kukutanisha wafanyabiashara wa ndani na wale wa kimataifa.

Matokeo ya mkakati huo yameendelea kuonekana ambapo kwa mwaka 2023 miradi ya uwekezaji iliongezeka kufikia 526 kutoka miradi 293 mwaka 2022, uwekezaji ambapo utazalisha ajira kwa maelfu ya Watanzania, utachochea ukuaji wa biashara, mzunguko wa fedha na kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Katika ziara yake ya kihistoria ya kitaifa nchini Norway Mheshimiwa Rais ameendeleza mkakati huo ambapo akizungumza katika Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Norway ametaja sababu za Tanzania kuwa eneo zuri kwa uwekezaji ikiwa ni pamoja na ukweli kuwa itakuwa moja ya nchi 20 duniani ambazo uchumi wake utakua kwa kasi zaidi mwaka 2024 kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Aidha, sababu nyingine ni amani chini ya demokrasia imara wa mfumo wa vyama vingi wenye kuzingatia tunu za utawala bora, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria. Kijiografia, amesema Tanzania inafaa kwa uwekezaji kwani ina Bandari ya Dar es Salaam katika Bahari ya Hindi, inayohudumia mataifa nane na ina usimamizi madhubuti wa uchumi na sera ya fedha.

Rais Samia amesisitiza fursa tano za kipaumbele zikiwemo uwekezaji katika nishati mbadala, kilimo, mafuta na gesi, mifuko ya uwekezaji, miundombinu na usafirishaji.

Tanzania na Norway zinaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano ambapo katika mazungumzo ya Rais Samia na viongozi waandamizi wa taifa hilo wamefikia makubaliano ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi kuendana na ukubwa wa historia ya uhusiano uliopo.