𝗛𝗔𝗜𝗝𝗔𝗪𝗔𝗛𝗜 𝗞𝗨𝗧𝗢𝗞𝗘𝗔: Tanzania yapata uwekezaji wa trilioni 4 ndani ya miezi mitatu

  • 𝐓𝐡𝐚𝐦𝐚𝐧𝐢 𝐲𝐚 𝐮𝐰𝐞𝐤𝐞𝐳𝐚𝐣𝐢 𝐢𝐦𝐞𝐨𝐧𝐠𝐞𝐳𝐞𝐤𝐚 𝐤𝐰𝐚 𝐚𝐬𝐢𝐥𝐢𝐦𝐢𝐚 𝟖𝟎
  • 𝐃𝐢𝐩𝐥𝐨𝐦𝐚𝐬𝐢𝐚 𝐲𝐚 𝐔𝐜𝐡𝐮𝐦𝐢 𝐧𝐚 𝐮𝐢𝐦𝐚𝐫𝐢𝐬𝐡𝐚𝐣𝐢 𝐦𝐚𝐳𝐢𝐧𝐠𝐢𝐫𝐚 𝐲𝐚 𝐛𝐢𝐚𝐬𝐡𝐚𝐫𝐚 𝐧𝐝𝐢𝐳𝐨 𝐬𝐢𝐫𝐢 𝐳𝐚 𝐦𝐚𝐟𝐚𝐧𝐢𝐤𝐢𝐨

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.4 (takribani TZS trilioni 4) ndani ya miezi mitatu ya mwisho ya mwaka jana, sawa na ongezeko la 80% ikilinganishwa na miradi yenye thamani ya dola za Marekani milioni 769.6 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2022.

Ongezeko hilo kubwa la uwekezaji limetokana na ziara za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan nje ya nchi ambazo zimevutia wawekezaji kupitia utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi na kuimarishwa kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ambayo yamevutia wawekezaji wengi zaidi.

Katika ziara hizo Mheshimiwa Rais Samia amekuwa akiambatana na wafanyabiashara kutoka Tanzania ambao hupata wasaa wa kuzungumza na wafanyabiashara kwenye nchi anazokwenda, hatua ambayo hutoa fursa ya kuwepo ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati yao.

Ripoti mpya ya TIC inaonesha kuwa miradi 161 ilisajiliwa kati ya Oktoba-Desemba 2023 ikilinganishwa na miradi 58 kwenye kipindi kama hicho mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 178, ambapo sekta tano zilizoongoza kwenye uwekezaji huo ni viwanda, usafirishaji, huduma, kilimo na utalii.

Miradi iliyosajiliwa Oktoba-Desemba 2023 inatarajiwa kutengeneza jumla ya ajira mpya 18,390, kutoka ajira 10,216 za kipindi kama hicho kilichopita kwa mwaka 2022 ambapo mikoa iliyoongoza kwa uwekezaji mkubwa ni Dar es Salaam na Pwani.

Aidha, ili kutoa fursa pia kwa wawekezaji wa ndani, pamoja na mambo mengine TIC imeanzisha kampeni maalumu ya kukuza uwekezaji wa ndani lengo likiwa ni kusajili miradi ya uwekezaji wa ndani yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.5 (TZS trilioni 9) ifikapo mwaka 2028.