Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu imeendelea kuleta mageuzi kwenye miradi ya kimkakati ambapo mradi uliosubiriwa kwa muda mrefu wa magadi soda wenye thamani ya zaidi ya TZS trilioni 1 (USD 400 milioni) katika eneo la Engaruka, wilayani Monduli mkoani Arusha umefufuliwa ambapo Serikali imeanza kuhamasisha wawekezaji kwenye mradi huo.
Katika kudhihirisha azma yake ya kuona mradi huo wenye tija kwa wananchi na taifa unaanza kutekelezwa mara moja, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameidhinisha kutolewa kwa zaidi ya TZS bilioni 14 ambazo zitalipwa kwa wananchi takribani 300 ambao watapisha mradi huo.
Kwa sasa serikali inatumia zaidi ya TZS bilioni 1 kwa mwaka kuagiza magadi soda toka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya malighafi hiyo viwandani, hivyo mradi huo utaokoa fedha hizo na kukuza mzunguko wa fedha ndani ya nchi pamoja na kutoa ajira za moja kwa moja 1,000, kukuza biashara na uchumi wa Taifa na kupunguza gharama za uzalishaji, hivyo kushusha gharama za bidhaa.
Hadi sasa wawekezaji zaidi ya 10 kutoka nchi mbalimbali wameonesha utayari wa kuwekeza kwenye mradi huo ambapo pia utaliwezesha Taifa kunufaika na uhawilishaji wa teknolojia, stadi na ujuzi kupitia wananchi watakaopata ajira.
Magadi soda hutumika zaidi katika uzalishaji wa vioo, mbolea, rangi (dye), sabuni, nguo, vyakula na vinywaji na dawa, hivyo uwepo wa malighafi hiyo utatochea uanzishwaji wa viwanda vya bidhaa mbalimbali ambazo zitauzwa katika soko la ndani na soko la nje, mathalani katika Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ambalo Tanzania imeanza kunufaika nalo.
Mradi wa magadi soda wa Engaruka ni moja kati ya miradi kumi na saba ya kimkakati ya Serikali iliyo chini ya Shirika la Taifa la Maendeo (NDC), ambao unakadiriwa kuwa na akiba ya magadi soda tani milioni 400.3 ambayo yatachimbwa kwa miaka 150 ijayo.