Moja ya falsafa za uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ni Mageuzi (Reforms) ambapo mwaka 2023 yalifanyika makubwa ikiwemo kuanzisha wizara mpya, mageuzi ndani ya wizara, kuanzishwa kwa Tume ya Mipango pamoja na mitaala ya elimu.
Mageuzi hayo yanaendelea mwaka 2024 ambapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuanzia Januari 2024 itaanza kutumia mfumo unaotumia riba katika kutekeleza Sera ya Fedha, badala ya mfumo unaotumia ujazi wa fedha, mabadiliko ambayo yanalenga kuongeza ufanisi wa sera ya fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha shughuli za kiuchumi.
Awali BoT katika utekelezaji wa Sera ya Fedha (kusimamia uchumi, mfumuko wa bei, mzunguko wa fedha, thamani ya shilingi na ustawi wa sekta ya fedha) ilifanya hivyo kwa kutumia kiwango cha fedha kilichopo mtaani (kwenye mzunguko), ambapo ilipunguza fedha kwenye mzunguko au kuziongeza kutokana na hali ya wakati huo, mfano mfumuko wa bei.
Katika mfumo mpya wa kutumia riba, ambayo itafahamika kama Riba ya Benki Kuu (CBR), BoT itatekeleza majukumu yake kwa kupandisha au kushusha kiwango cha riba kwa mikopo kwenda benki za kibiashara, ili kuongeza au kupunguza fedha kwenye mzunguko au kukabiliana na changamoto nyingine ya kiuchumi kwa wakati husika.
Kwa kutumia mfumo wa CBR, benki kuu inatekeleza makubaliano ya kutumia mfumo mmoja wa utekelezaji wa sera ya fedha katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya nyingine za kiuchumi ambazo Tanzania ni mwanachama.
Mbali na kuhakikisha ukwasi katika uchumi, kukuza uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei, riba hiyo itatumika pia kama kiashiria kimojawapo katika upangaji wa riba zinazotozwa na mabenki na taasisi nyingine za fedha nchini. Hii ikimaanisha kuwa, kadiri riba ya BoT itakavyozidi kuwa ndogo, kutatoa uwezekano mkubwa kwa wananchi kupata mikopo kwa riba nafuu zaidi.
Hata hivyo, BoT imesisitiza kuwa riba yake haimaanishi kuweka ukomo katika viwango vya riba zinazotozwa na benki na taasisi nyingine za fedha nchini, na kwamba kiwango cha riba za mikopo kwa wananchi kitaendelea kuamuliwa na nguvu ya soko, kuendana na sera nyingine za kiuchumi nchini.