Tanzania imeweka mkakati wa kutumia mageuzi ya kilimo kupunguza umaskini wa wananchi ikizingatiwa kuwa takribani asilimia 70 ya Watanzania wanategemea sekta hiyo. Akizungumza katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Usalama wa Chakula, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amesema Tanzania imekuja na Ajenda ya 10/30 ambayo inalenga kuwezesha kilimo kukua kwa asilimia 10, kutoka asilimia 4 ya sasa, ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Rais ametaja hatua ambazo Serikali imechukua na inaendelea kuchukua ikiwa ni pamoja na kutoa vivutio vya kikodi kwa sekta binafsi ili ishiriki kikamilifu kwenye kilimo. Vivutio hivyo ni pamoja na kutoa punguzo la kodi (capital allowance) kwa asilimia 100, kusamehe ushuru wa forodha na kodi ya ongezeko la thamani katika vifaa vya kilimo ikiwemo vya vifaa vitakavyotumika katika umwagiliaji, uongezaji thamani, kulima na nishati salama, hatua ambayo inalenga kupunguza gharama za uwekezaji.
Hatua nyingine ni Mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT) kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kufanya kilimo cha kisasa, mradi ambao utawezesha kuongeza uzalishaji na kutunza mazingira. “Kutunza mazingira bila kupunguza umaskini tutakuwa tunafanya kazi bure,” amesema huku akiongeza kuwa kazi ya Serikali ni kuwapa vijana mafunzo na ardhi, hivyo sasa sekta binafsi inatakiwa iingie kwenye kutoa fedha, lakini pia mitambo kufanya kilimo chetu kiwe cha kisasa
Pia, amebainisha kuwa mkazo umewekwa katika tafiti ili kuwezesha wananchi kufanya kilimo chenye uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko, ukame, wadudu na kutunza mazingira. Katika eneo hili Serikali imejenga na inahamasisha sekta binafsi kujenga skimu za umwagiliaji na mabwawa ya kuvuna maji ya mvua.
“Sekta binafsi itakuwa na kazi ya kuhakikisha wanaongeza thamani mazao yote yanayozalishwa, lakini pia biashara ya kilimo,” amesema Mheshimiwa Rais na kuongeza kuwa katika hili Serikali inahakikisha upatikanaji wa ardhi na utoaji wa leseni na vibali kwa wawekezaji wanaotaka kuingia kwenye kilimo cha kisasa na nishati salama.
Akitambua kuwa mtaji ndio changamoto kubwa, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetenga TZS bilioni 150 ambazo zinatolewa na benki za kibiashara kupitia madirisha maalum ya mikopo ya kilimo na biashara za kilimo ambapo tayari wananchi wameanza kunufaika na urejesha wa mikopo hiyo ni mzuri.
Katika kupunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje, Tanzania imeziwezesha taasisi za utafiti kuwa na mashamba ya kuzalisha mbegu na kufanya tafiti ya mbegu bora, ambapo mbegu zitakazopitishwa zitakabidhiwa kwa sekta binafsi kwa ajili ya uzalishaji zaidi na usambazaji kwa wakulima.
Hatua hizi zinazochukuliwa pamoja na mambo mengine zinalenga kutengeneza ajira mpya milioni tatu za vijana na wanawake ifikapo mwaka 2030 na kuongeza thamani ya mauzo nje ya nchi kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 hadi dola za Marekani Bilioni 5 ifakapo mwaka huo.