Katika kuendelea kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji hasa kutoka nje ya Tanzania kutumia Bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yao, Serikali ya Tanzania imetenga hekta 20 za ardhi katika Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani kwa ajili ya mizigo inayokwenda Zambia, ikiwa ni sehemu ya kurahisisha ufanyaji biashara.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa Zambia katika Bandari ya Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa mizigo inayokwenda nchini humo itakuwa na kipindi cha neema (bure) kirefu zaidi cha kuhifadhi mizigo yao hadi siku 45, ikiwa ni mkakati wa kupunguza msongamano na ucheleweshaji, na hivyo kupunguza gharama za biashara.
Mheshimiwa Rais Samia alisema hayo akihutubia katika maadhimisho ya miaka 59 ya uhuru wa Zambia ambapo alikuwa mgeni rasmi, na kuongeza kuwa “tunatarajia kuwa hatua hii itaongeza biashara kati ya nchi zetu mbili na kuzalisha fursa zaidi kwa ajili ya wananchi wetu. Hii ni zawadi kutoka kwa Tanzania mkisherehekea uhuru wenu.”
Zambia ni nchi ye pili kwa kupitisha shehena kubwa ya mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam baada ya DR Congo ambapo kwa mwaka 2022 ilipitisha tani milioni 1.98, sawa na asilimia 24 ya mizigo yote iliyokwenda nje. Aidha, ifahamike kuwa asilimia 80 ya mizigo yote inayopita bandari ya Dar es Salaam kwenda nje ya nchi, inapita katika mpaka wa Zambia, jambo linaloifanya nchi hiyo kuwa mshirika wa kimkakati.
Uamuzi wa Mheshimiwa Rais Samia umekuja wakati ambapo Tanzania imeanza mageuzi ya kiutendaji katika Bandari Dar es Salaam yatakayowezesha kupokea meli kubwa zaidi na kutoa huduma kwa kasi, hivyo inaihitaji sana Zambia kuwa na imani na mazingira mazuri ya biashara ili iendelee kuitumia bandari hiyo, badala ya kugeukia bandari shindani.
Mbali na bandari, Mheshimiwa Rais Samia ameeleza azma ya Serikali yake kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika ukanda wa kusini na ukanda wa mashariki ili kuongeza usambazaji wa umeme kwenye maeneo hayo. Pia, amesema Zambia na Tanzania zitaendelea na mkakati wa kuimaisha bomba la mafuta la TAZAMA na kujenga bomba la gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Zambia.