Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali anayoiongoza inatambua na kuthamini mchango wa wachimbaji wadogi katika kuzalisha ajira nchini, na ameahidi kuwa ataendelea kuwaunga mkono kwa kuboresha mazingira ya uchimbaji pamoja na biashara ya madini ili waweze kuboresha maisha yao na kuchangia kwenye uchumi wa taifa.
Ametoa ahadi hiyo leo wakati akizindua vifaa vya uchimbaji madini vilivyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambapo ni pamoja mitambo mitano ya kuchoronga, ambayo inatarajiwa kuongezwa kufikia 15 ifikapo Juni 2024. Mitambo mingine ni mitambo 10 ya kutwanga mawe yanayoaminika kuwa na dhahabu, mitambo mitatu ya kuzalisha mkaa mbadala pamoja na makontena ya kusambaza mkaa huo na magari ya STAMICO.
Mitambo hiyo ambayo itatumiwa na wachimbaji wadogo nchi nzima itawapunguzia gharama, mfano mtambo wa kuchoronga sasa utakodishwa kwa bei nafuu ikilinganishwa na gharama ya TZS 375,000 ambayo walitozwa na wamiliki binafsi kwa kuchoronga kwa kila mita moja. Mitambo ya kutwanga mawe itaongeza uwezo wao kutoka tani 2 za sasa kwa siku hadi tani 12 kwa siku.
Kununuliwa kwa mitambo hiyo ni mwendelezo wa mikakati ya serikali kuwainua wachimbaji wadogo ambapo hatua nyingine zilizochukuliwa ni kufutwa kwa kodi ya ongezeko la thamani ya asilimia 18 pamoja na kodi ya zuio ya asilimia 5 kwa wachimbaji wadogo watakaouza madini yao kwenye masoko ya ndani ya nchi.
Kama haitoshi, serikali pia imetoa punguzo la asilimia mbili la mrahaba pamoja na kuondoa asilimia 1 ya ada ya ukaguzi wa madini kwa wachimbaji wa dhahabu ambao wengi wao ni wachimbaji wadogo.
“Hii ina maana wale watakaouza dhahabu kwenye viwanda hivyo watapata punguzo la asilimia tatu ya tozo za serikali kwenye mauzo ghafi ya madini yao,” amesema Mheshimiwa Rais Samia akiongeza kuwa hatua hizo ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyoielekeza serikali kubuni na kuendeleza mikakati ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa tija.
Serikali haikuishia hapo, bali pia inatoa huduma za utafiti kwa gharama nafuu, mafunzo kuhusu uchimbaji na biashara ya madini kupitia vituo vya kisasa, kufikisha umeme kwenye maeneo ya machimbo na kuwawezesha kupata mikopo na mitaji.