Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweka wazi kuwa Tanzania inalenga kusajili miradi ya uwekezaji kutoka nje (FDI) yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 15 (TZS trilioni 37.5) ifikapo mwaka 2025.
Ameweka wazi mpango huo wakati akizungumza na wafanyabiashara wakubwa wa India katika jukwaa la uwekezaji la India na Tanzania jijini New Delhi ambapo amesema ili kufanikisha azma hiyo Serikali yake imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuboresha mfumo wa kisheria kwa kuufanya kuwa rafiki zaidi.
Ameeleza kuwa Serikali yake inatambua umuhimu wa sekta binafsi na uwekezaji kama vichocheo vya ukuaji wa kiuchumi, hivyo mazingira ya biashara yameboreshwa ili kupanua biashara zilizopo na kuvutia uwekezaji mpya, jambo ambalo ni moja ya malengo ya ziara yake ya kimkakati nchini India.
Kama sehemu ya mageuzi makubwa, Tanzania imeboresha matumizi ya teknolojia kuruhusu wawekezaji kusajili miradi popote pale duniani kupitia dirisha la kuhudumia wawekezaji kielektroniki, na hivyo kupata majibu kabla hata ya kutembelea Tanzania.
“Tumepiga hatua kutoka kusajili uwekezaji wa dola bilioni 2 [TZS trilioni 5] mwaka 2020 hadi dola bilioni 5 [TZS trilioni 12.5] katika mwaka ulioishia Juni 2023. Lengo letu ni kufikia dola bilioni 15 kwa mwaka ifikapo mwisho wa 2025,” amesema.
Tangu mwaka 1997 Tanzania imepokea jumla ya dola bilioni 3.87 za uwekezaji katika miradi 675 kutoka India ambayo imezalisha ajira zaidi ya 61,000, hivyo kufanya India kuwa miongoni mwa wawekezaji watano bora nchini Tanzania.