Tanzania imeendelea kutekeleza sera yake ya Diplomasia ya Uchumi inayolenga kujenga na kuimarisha uhusiano wake wa kimataifa na kujenga mahusiano ya kibiashara na kiuchumi na taasisi pamoja na mataifa mengine ili kuchochea maendeleo.
Historia nyingine imeandika baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kushiriki na kuhutubia katika Mkutano wa 15 wa BRICS (Brazil, Russia, India, China, South Africa) ambalo ni jukwaa la nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi duniani ambapo pato la Taifa la mataifa hayo ni quadrilioni TZS 63.3, ambapo pia kutokana na kupokea wanachama wapya sita, kuanzia Januari 2024 nchi sita kati ya tisa zinazozalisha mafuta zaidi duniani zitakuwa mwanachama wa jukwaa hilo.
Kwa kushiriki kwenye mkutano huo, Tanzania itapata manufaa makubwa kiuchumi na kibiashara kwani kunaiwezesha kujenga mahusiano ya kiuchumi na biashara na nchi hizo zenye nguvu hatua inayoweza kufungua fursa mpya au kupanua fursa zilizopo za kuuza bidhaa za Tanzania kwenye masoko ya nchi hizo, na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi. Ni wazi pia kuwa mataifa ya BRICS yamepiga hatua kwenye teknolojia, hivyo Tanzania inaweza kujifunza matumizi bora ya teknolojia katika kurahisisha utoaji huduma na kuchochea maendeleo.
China ambayo ni mwanachama wa BRICS ni mshirika mkubwa maendeleo wa Tanzania ambapo kwa miezi saba ya mwaka 2023 imeongoza kwa uwezekaji (Foreign Direct Investment) nchini ikiwekeza mtaji wa zaidi ta TZS trilioni 1.2 ambao pamoja na mambo mengi utazalisha ajira kwa maelfu ya Watanzania. Katika mkutano huo Rais Samia alipata nafasi ya kuzungumza na Rais wa China, Xi Jinping, ikiwa ni mara nyingine kwa viongozi hao kukutana baada ya ziara ya Rais Samia nchini China. Mazungumzo hayo huenda yakaongeza uwezekano wa kufadhili miradi muhimu kama miundombinu, nishati, kilimo, na teknolojia, uwekezaji pamoja ushirikiano wa kiusalama.
Katika dunia ya sasa, nchi haiwezi kujitenga kama kisiwa, inailazimu kutoka, kukutana na kushirikiana na mataifa mengine ili kufanikisha masuala mbalimbali yenye kuchochea maendeleo na ustawi wa Taifa husika. Kwa muktadha huu, utayari wa Tanzania kushiriki kwenye mkutano huo unatuma ujumbe kwamba Tanzania ipo tayari kushirikiana na mataifa mengine ambayo pia yataiunga Tanzania mkoano kwenye masuala ya kimataifa, mfano inapokuwa na mgombea anayehitaji kuungwa mkono hasa wakati wa uchaguzi.
Pia, ni jukwaa muhimu kwa Tanzania kueleza na kushiriki kujadili masuala au changamoto zinazohitaji utatuzi wa pamoja. Mfano, katika hotuba Mheshimiwa Rais Samia alieleza kuwa Tanzania inaweka mkazo kwenye kufanya maboresho kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuwa na uwakilisha sawa, ufanisi na liakisi hali ya sasa ya siasa za kimataifa. Hili lilikuwa ni jukwaa sahihi kwa ujumbe huu kwani linatoa uhakika wa ujumbe kufika mbali zaidi, tofauti na endapo ujumbe huo ungetolewa kwenye matukio ya kitaifa.
Ni wazi kuwa karne ya 21 inayaita mataifa kushirikiana zaidi kwa manufaa ya pande zote kwani changamoto zilizopo duniani kwa sasa hazitatuliki kwa kila Taifa kujifungia na kufanya kwa kivyake na wala fursa zilizopo hazitalinufaisha Taifa endapo litajitenga na wengine.