USAID yampongeza Rais Samia kwa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa

Mageuzi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii anayoendelea kuyafanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa manufaa ya Watanzania wote yameendelea kuwavutia wengi wanaopongeza juhudi zake ambapo mwisho wa wiki Msimamizi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Bi. Samantha Power ametoa pongezi zake kwa Rais kwa juhudi zake katika kuendeleza mageuzi ya kidemokrasia na ushirikishwaji wa wananchi.

Bi. Power amesema kuwa jitahda za Rais Samia zimewezesha Tanzania kupanua ushirikiano wa kimaendeleo na kuifanya iwe rahisi kwa sekta binafsi ya Marekani kuizingatia Tanzania kama mahali pazuri pa kuwekeza.

Aidha, ameeleza kuwa kazi ya kuvutia uwekezaji na biashara itakuwa rahisi Tanzania ikiendelea na mageuzi katika maeneo ya utawala na kusisitiza kuwa makubaliano ya malengo ya maendeleo yanatoa fursa ya kuongeza mara mbili zaidi mafanikio yaliyopatikana katika ushirikiano imara kati ya nchi hizo mbili.

Amempongeza Rais pia kwa ushirikishwaji wa wananchi, hususani vijana, katika shughuli za maendeleo akisema tofauti na maeneo mengine ambayo vijana huchukuliwa kama Taifa la kesho, kwa Tanzania vijana ndio Taifa la sasa. Kupitia ujenzi wa uchumi shirikishi kwa kutumia teknolojia ameeleza imani yake kuwa Tanzania itanufaika kwani wananchi wake wengi ni vijana.

Pongezi zaidi amezitoa kwa Rais kwa namna Tanzania inavyotumia teknolojia kupitia Programu ya M-Mama inayowawezesha wajawazito kupata huduma zinazowawezesha kuokoa maisha yao, hasa katika maeneo ya vijijini ambapo hadi sasa imepunguza vifo vya uzazi kwa asilimia 38.