Dhamira za dhati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta binafsi na kuhakikisha inashiriki katika kuchochea maendeleo ya wananchi inazidi kudhihirika kufuatia marekebisho yaliyofanyika kwenye Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2023 ili kuondoa changamoto zilizosababisha ushiriki hafifu wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa utaratibu wa ubia.
Maboresho yaliyofanyika yataongeza kasi ya ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kupunguza muda wa maandalizi ya miradi na hivyo kuharakisha utekelezaji wa miradi ya PPP, hatua ambazo zitaipunguzia Serikali mzigo wa kibajeti sambamba na kukuza sekta binafsi.
Changamoto zilizotatuliwa ni pamoja na sheria kutotoa haki kwa wabia kutoka sekta binafsi kuwasilisha migogoro kwenye mahakama za kimataifa kwa utatuzi, kutoainisha aina ya misaada ya kifedha (public funding) itakayoidhinishwa kupitia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada.
Nyingine ni sheria kutoruhusu mamlaka za Serikali kufanya ununuzi wa moja kwa moja wa mbia kutoka sekta binafsi kwa ajili ya kutekeleza miradi inayoibuliwa na mamlaka hizo na kutoweka masharti kwa mwekezaji kutoka sekta binafsi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa PPP kuunda Kampuni.
Tayari Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo barabara (Expressway) kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro, mradi ambao utaweka historia ya kuwa mradi mkubwa zaidi wa barabara kujengwa kwa kushirikiana na sekta binafsi.