Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anaiunda upya Tume ya Mipango ambayo itakuwa chini ya Rais ikiwa na jukumu la kubuni, kupanga, kuratibu na kusimamia mipango ya maendeleo ili kuwa na mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.
Kuunda upya kwa tume hiyo na kuiweka chini ya Rais ni kuendelea kuyaishi maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye kwa mara ya kwanza alianzisha mwaka 1962 ikiwa ni idara ambapo wakati wa uanzishaji wake walisema “Nakusudia kuanzisha idara mpya, idara ya mipango ya maendeleo, idara hiyo itakuwa chini yangu mwenyewe.”
Uamuzi wa Rais kurejesha tume hiyo utawezesha uwepo wa utaratibu wa kupanga pamoja mipango ya kisekta, hususani sekta zenye majukumu yanayotegemeana na kuwa na mfumo wa kisheria na chombo mahsusi cha kusimamia uandaaji, utekkelezaji wa mipango ya maendeleo, utafiti na kuishauri Serikali kuhusu vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.
Majukumu haya kwa sasa yanatekelezwa na Wizara ya Fedha na Mipango, lakini kumekuwepo na changamoto ya miradi inayoendana kutekelezwa kwa nyakati tofauti sehemu husika, mfano barabara inajengwa baada ya muda inavunjwa ili kupitisha bomba la maji. Hivyo kuwepo kwa tume maalum chini ya ofisi ya Rais kutaondoka mkanganyiko huo ili miradi kama hiyo itekelezwe kwa wakati mmoja ili kuleta ufanisi na kuipunguzia serikali gharama zisizo za lazima.
Aidha, tofauti na tume iliyokuwepo awali ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa hati idhini (instruments) tume mpya itakuwa na hadhi ya kisheria ambayo itaipa tume nguvu zaidi na kulinda mawazo yanayotolewa na kuleta utofauti katika mfumo wa uendeshaji.